Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi James Kilaba.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa
simu za mkononi kutorudisha pesa kwa mtu aliyetuma kimakosa.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mtakwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), Batholomew Marcel wakati akiwasilisha mada iliyohusu
ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano na tahadhari za kuzingatiwa na mtumiaji
wa Huduma na bidhaa za mawasiliano katika warsha kuhusu Mradi wa Kukuza
Utawala Bora na uwajibikaji Tanzania kupitia teknolojia ya dijitali,
iliyofanyika Dar es Salaam jana.
“KAMA kuna pesa imetumwa kimakosa kwenye simu yako, hata kama mwenye
simu aliyekutumia kimakosa atakuomba na kukubembeleza, usimrudishie
yeye, bali ziache na uijulishe kampuni ya simu inayohusika wao ndio
wamrudishie” alisema Batholomew.
Aliwatahadharisha watanzania kua makini kwani hali hiyo inaweza
kuwasababishia hasara na pengine kuwaingiza katika mikono ya sheria za
nchi kama tuhuma za uhalifu mwingine wowote, licha ya kua na nia nzuri
ya kurudisha pesa.
Alisema anayepokea pesa iliyotumwa kwake kimakosa anapaswa kuijulisha
kampuni husika ya simu vinginevyo anaweza kujikuta anafanya malipo na
kutuma pesa kwa wahalifu huku mifumo ikionesha pesa ilikwenda kwake.
Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano
(ICT), watu wengi wanatumia simu kutunza, kupokea na kutuma pesa zao
hivyo, mikakati bora zaidi haina budi kuwapo ili kuepusha uhalifu wa
kimtandao hususani kuhusu pesa mtandao.
“Hapa lazima kuwa makini kwani teknolojia hii ya pesa mtandao pia ina
changamoto nyingi na hatari. Kazi ya kurudisha pesa kwa aliyetuma
kimakosa, iache ifanywe na kampuni husika ya simu yaani mtoa huduma sio
wewe,” alisema.
Changamoto nyingine Marcel alisema ni pamoja na kuibuka wimbi la
matapeli wanaojifanya kumfahamu mtu huku wenyewe wakijifanya ni
wanasiasa, viongozi wa kikazi, kiserikali, kidini au wanafamilia
wanaotoa maelekezo ya kumtaka mtu afanye malipo, kutuma pesa au kuhitaji
msaada kwa ulaghai.
Aliwataka watumiaji wa huduma hizo kuwa makini kwani makosa ya
kimtandao ni makosa kama yalivyo mengine na yana sheria zake ikiwamo
Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.
Akasema, “Epuka kutunza pesa nyingi katika chombo kimoja kama simu,
ukipoteza simu toa kwanza taarifa kwa kampuni husika ya simu ili
waifunge kisha sasa, toa taarifa polisi na pia, badili password (namba
ya siri) mara kwa mara walau kila baada ya siku 90.”
Akaongeza, “Wengine wanaokumbwa au kulizwa na changamoto za pesa
mtandao, ni wale wanaokubali kuaminishwa kuhusu kuwapo biashara inayozaa
faida kubwa kwa muda mfupi, kushinda bahati nasibu hata ambazo
hawakushiriki na kupata mikopo kirahisi, lakini wakatakiwa kutanguliza
malipo,” alisema.
Akasisitiza, “Kuwa makini kwa kuepuka mikopo au dili zinazokutaka
kutanguliza fedha…” Kwa upande mwingine, alisema zipo fursa nyingi za
mitandao ikiwamo kufanya malipo mbalimbalimbali yakiwamo ya huduma za
kijamii kama maji, umeme na ankara nyingine; pamoja na biashara huku
wengine wakijiajiri au kuajiriwa katika sekta hiyo ya pesa mtandao.
Katika hatua nyingine, Afisa wa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHCR), Pasience Mlowe, katika warsha hiyo aliiomba Serikali
na watunga sera na sheria kuzitazama upya sheria alizosema ni kandamizi
ikiwamo Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya Mwaka 2015.
Katika taarifa kuhusu namna Oxfam inavyotumia ICT duniani, Bill Marwa
alisema ni pamoja na kuwatumia watu wanaowasaidia na kukusanya pesa
toka kwa wafadhili mbalimbali. “Teknolojia hii inatusaidia kuokoa muda
na pesa,” alisema.
Comments
Post a Comment