Thanda: Kisiwa kinachopatikana Tanzania ambapo kulala usiku mmoja inagharimu zaidi ya shilingi milioni 22!
Inawezekana
usiamini kwamba kuna sehemu zinagharimu zaidi ya shilingi milioni 22 za
kitanzania kulala kwa usiku mmoja tu! Amini au usiamini sehemu hizo
zipo, tena hapa hapa nchini kwetu Tanzania.
Jumia Travel
ingependa kukujulisha kwamba kupitia shughuli za kitalii, hakuna
kinachoshindikana. Linapokuja suala la kujionea mazingira adimu na ya
kuvutia au wanyama wa aina mbalimbali, gharama au umbali wa
kuyafanikisha hayo huwa siyo masuala ya msingi.
Thanda,
ni sehemu kwa ajili ya mapumziko iliyotengenezwa na mtu binafsi katika
eneo la kisiwa cha Shungimbili kilichomo Wilaya ya Kisiwa cha Mafia.
Kisiwa hiki kina ukubwa wa takribani hekari 20 ambamo ndani yake
imejengwa nyumba moja. Nyumba hiyo ina vyumba vya kulala vitano na
vibanda viwili pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi kusini mwa
Tanzania ambapo familia ya watu mpaka 10 inaweza kuishi.
Ili
kuweza kuishi kwenye kisiwa hiki, wamiliki hutoza wageni kiasi cha dola
za kimarekani 10,000 kwa usiku mmoja ambazo ni zaidi ya shilingi
milioni 22 za kitanzania. Mazingira ya kuvutia, utulivu wa hali ya juu
na namna eneo hili lilivyotengenezwa ndivyo vinavyowafanya watalii
kulipia gharama hizo lisiwe ni jambo la kushangaza. Ni jambo la kawaida
ukiwa mapumzikoni kisiwani humo kuwaona au kuogelea pamoja na viumbe wa
baharini kama vile pomboo (dolphin), papa wakubwa (whale sharks) na kobe
wa majini.
Wamiliki
wa kisiwa hiki binafsi cha mapumziko, wanandoa Bw. Dan na Bi. Christin
Olofsson ambao asili yao ni Sweden walipata wazo la kutengeneza sehemu
hii ikiwa ni kwa ajili ya kupumzikia pamoja na watoto wao watatu na
wajukuu nane. Kikubwa kilichowasukuma kufanya hivyo ni katika jitihada
za kubadili mazingira hususani hali ya hewa ukizingatia nchi za
Scandinavia wanapotea hukumbwa na baridi kali kwa vipindi virefu vya
majira ya mwaka. Walianza kwa kuwekeza Afrika ya Kusini kutokana na
kuvutiwa na wanyama na uoto wa asili kabla ya kuja nchini Tanzania.
Miongoni
mwa masuala ambayo yalizingatiwa kabla ya uwekezaji katika kisiwa hiki
ni pamoja na kulinda vivutio vya kitalii na kuhifadhi viumbe wa baharini
katika eneo hilo. Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uhifadhi wa Baharini
ya Kisiwa cha Shungimbili, wamiliki wa Kisiwa cha Thanda wanashirikiana
kwa ukaribu kuhakikisha jitihada za kulinda na kuendeleza uhifadhi wa
vivutio vyake unazingatiwa.
Mbali
na hayo, Kisiwa cha Thanda kinahakikisha kwamba jamii ya wakazi
wanaoishi karibu na sehemu hiyo ambapo ni Kisiwa cha Mafia, wanafaidika
na uwekezaji huo. Wakazi wake wananufaika kupitia ajira, uchangiaji
kwenye shughuli za maendeleo ya elimu pamoja na uhifadhi wa viumbe wa
baharini ambalo ndio kipaumbele kubwa.
Tanzania
inazo fursa nyingi za kitalii ambazo watu kutoka mataifa ya nje
wanaziona na kuzitumia ipasavyo. Jumia Travel inaamini kwamba kupitia
makala haya utakuwa umejifunza mambo mengi kuhusu Kisiwa cha Thanda
ambayo hukuyajua hapo awali. Ni fursa kwako kuendelea kutafuta na
kujifunza vivutio vinavyopotikana sehemu nyingine za nchi.
Kipo vizuri Sana lakin mzawa shida kwenda kuenjoy maana bei ghali
ReplyDelete