Sababu 6 za kunywa maji yenye limao kila unapoianza siku yako



Na Jumia Food Tanzania

Kutokana na mabadiliko ya namna tunavyoishi hivi sasa suala la afya limekuwa ni jambo la msingi ambalo watu wengi wanalizingatia. Magonjwa yanayotokana na mienendo ya mifumo ya maisha watu wanayoishi sasa yamekuwa yakikua kwa kasi kiasi kwamba kampeni za afya zimekuwa zikishika hatamu kila kukicha.

Ukiachana na mazoezi au kupunguza kula aina fulani ya vyakula ili kuufanya mwili wako uwe wenye afya na kujikinga na baadhi ya maradhi, kuna baadhi ya tabia ambazo ukizianza sasa zinaweza kuwa na manufaa makubwa kwako. Jumia Food imekukusanyia faida 6 ambazo unaweza kuzipata kutokana na kuanza kunywa maji yenye limao kila unapoianza siku yako.  

Inasaidia mmeng’enyo wa chakula. Asidi zilizomo kwenye tumbo husaidia kuvunjavunja chakula tunachokula ili kumeng’enyeka kwa urahisi. Na kwa kunywa maji yenye limao asubuhi kunaweza kusaidia kuongeza asidi tumboni, ambazo hupungua kadri umri wetu unavyoongezeka.

Inasaidia mwili kuwa na maji. Maji hupotea mwilini kwa njia nyingi zikiwemo kutoka jasho, kukojoa, kutapika, kuharisha na kadhalika. Na kutokana na miongoni mwetu kuwa na mfumo wenye pilikapilka nyingi za kutafuta kipato, wengi huwa hatunywi maji ya kutosha kitu ambacho siyo kizuri kwa afya ya miili yetu. Hivyo basi, kwa kunywa maji yenye limao asubuhi husaidia mwili wako kuwa na maji.

Husaidia kuzuia mawe kwenye figo. Hii hutokana na mabaki ya madini na chumvi kwenye figo yanayojikusanya na kuwa vitu vigumu mfano wa mawe. Mojawapo ya sababu inayopelekea hali hii ni upungufu wa maji mwilini. Na uwepo wake mwilini huwa na madhara kama vile damu kwenye mkojo, maumivu wakati wa kukojoa nakadhalika. Hivyo, kwa kunywa maji yenye limao kila siku asubuhi kunaweza kusaidia kuzuia kutokea kwa mawe hayo kwenye figo mwilini.  

Huupatia mwili potasiamu inayohitajika. Haya ni madini muhimu ambayo mwili yanayahitaji ili uweze kufanya kazi ipasavyo. Potasiamu ni muhimu kwa mawasiliano ya mishipa ya misuli na kusafirisha virutubisho na taka mwili. Kwa kunywa maji yenye limao kila asubuhi kutasaidia mwili kupata potasiamu inayoihitaji.

Yana vitamini C ya kutosha. Kunywa maji yenye limao kila asubuhi kusaidia mwili kuupatia virutubisho vyenye vitamini C inayoihitaji, ambayo ni muhimu katika kulinda kuharibika kwa seli na kupona majeraha.

Husaidia kupunguza uzito wa mwili. Mbali na kuachana na tabia za kula aina za vyakula fulani au kufanya mazoezi ili kukusaidia kupunguza uzito wa mwili, pia kunywa maji yenye limao kila asubuhi ni tiba mbadala.

Zipo faida nyingi za kuanza kunywa maji yenye limao ambazo Jumia Food haiwezi kuziorodhesha zote hapa kama vile kusaidia kupunguza harufu mbaya ya kinywa. Faida mojawapo kwa watanzania wengi ni kwamba malimao yanapatikana kwa urahisi, gharama nafuu na takribani kipindi chote cha mwaka. Anza sasa kutumia limao kama tiba mbadala kwa afya ya mwili wako, naamini utaratibu huu utakuwa ni wenye manufaa kwako.


Comments