- Tunzo hizo zimefanyika kwa
awamu ya pili ambapo ni katika kuonyesha kujizatiti kwake kwenye sekta ya
huduma za hoteli na utalii
Kampuni inayojihusisha na huduma za usafiri kwa
njia ya mtandao barani Afrika, Jumia Travel, imeadhimisha awamu ya pili ya utoaji wa tunzo za hotel na usafiri
katika hafla fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, katika ukumbi wa hoteli ya Harbour
View Suites jijini Dar es Salaam.
Tunzo hizo zimelenga
kuzitambua na kuzitunuku hoteli, mashirika ya ndege na tovuti ambazo kwa namna
moja ama nyingine zimechangia mafanikio kwenye sekta ya usafiri, huduma za
hoteli, na utalii kwa mwaka 2017, pamoja na kuleta hamasa ya kutoa huduma bora
kwa Watanzania.
Akizungumza wakati wa
hotuba fupi ya ufunguzi kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Meneja Mkazi wa Jumia
Travel Tanzania, Meneja wa Uhusiano na Umma, Geofrey Kijanga alibainisha kuwa,
“ni dhahiri kwamba sekta ya usafiri na utalii barani Afrika imekua ikikua
kadiri miaka inavyokwenda, ambapo utolewaji wa huduma za hoteli na ndege
umehamia mtandaoni. Kutokana na mabadiliko hayo, watoa huduma hawana budi kutoa
huduma bora zaidi ili kutimiza mahitaji ya wateja wao.”
“Kwa kulitambua hilo,
Jumia Travel tumeandaa tunzo kwa ajili ya hoteli, mashirika ya ndege, na tovuti
mbalimbali ambazo zinaandika habari za kitalii, kuhamasisha utoaji wa huduma
bora, kuziwezesha jitihada za hoteli kuboresha huduma zao ili kufikia matarajio
ya wateja wao, pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia mpya katika utoaji wa
huduma za hoteli,” aliongezea Kijanga.
“Awamu ya pili ya utoaji
wa tunzo hizi, umelenga kuwakutanisha wadau kutoka pande zote mbili za huduma
za hoteli na utalii. Lengo kubwa ni kuutambua mchango wao na kuweka vigezo na
viwango vya ubora kwa sekta ya utalii Afrika, na nafasi ya Jumia Travel katika
jitihada hizi,” alisema na kumalizia, “Kwa ujumla, sherehe hizi zinakata kiu ya
kuwahamasisha na kuwahimiza wamiliki wa hoteli kuboresha huduma zao, kwani
hakuna kitu kama hiki kwa sasa. Lakini pia kutokana na ubora wa huduma zao
wataweza kuyatangaza maeneo waliyopo, kuboresha utaalamu ndani ya sekta, kukuza
hamasa ya matumizi ya njia za kidigitali, na kukuza sekta nzima ili kufikia
viwango vya kimataifa.”
Tunzo hizo ambazo
ziliwatunuku wadau wa huduma za hoteli na usafiri kwa mwaka 2017, zilijumuisha
vipengele saba ambavyo ni: Tunzo ya Hoteli Bora kutoka Jumia Travel (Amaan
Bungalows iliibuka washindi), Chaguo Bora la Wasafiri (Mazsons
iliibuka washindi), Hoteli Bora ya Kifahari (Park Hyatt Zanzibar
iliibuka mshindi), Hoteli Bora ya Kibiashara (Harbour View Suites
iliibuka mshindi), Hoteli Pendwa na Wateja (Hotel White Sands:
Beach Resort iliibuka washindi), Shirika Bora la Ndege (Precision
Air iliibuka washindi), na Tovuti Bora ya Kitalii (Michuzijr
Blogspot iliibuka mshindi).
Wakati akipokea tunzo ya
Hoteli Bora ya Kibiashara, Meneja Mapokezi wa Harbour View Suites, Hemed
Kiwanga alielezea furaha yake kwa kutunukiwa tunzo hiyo kwa mara ya kwanza
kwamba ni ishara nzuri kuwa jitihada za utoaji wa huduma zao zinaonekana.
“Sikutarajia jioni hii kama
hoteli yetu ingekuwa ni miongoni mwa washindi kwani kipengele tulichokuwemo
kilikuwa na ushindani mkubwa. Nadhani tumestahili kupata tunzo hii kwani hoteli
yetu ipo katika mazingira mazuri ya kibiashara, katikati kabisa ya jiji la Dar
es Salaam, huku tukiwa na huduma zote ambazo mteja akija kwa shughuli za
kibiashara anazipata,” alisema na kumalizia, “Nawashukuru tena Jumia Travel kwa
tunzo hii na jitihada zao za dhati ambazo ni hamasa kwa wadau wa hoteli
kutojisahau, kuendana na matakwa ya wateja pamoja na soko la sasa. Kwa
wasioshinda kwenye awamu hii ningependa kuwatia moyo kutokata tamaa badala yake
waone kama ni fursa ya kujipanga zaidi na kujifunza kutoka kwa washindi ni vitu
gani vilivyopelekea mpaka kutunukiwa tunzo hizi ili nao waibuke washindi
kipindi kijacho.”
Katika hafla hiyo fupi
Jumia Travel iliweka wazi mipango yake katika kusukuma mbele zaidi sekta ya
huduma za hoteli na utalii nchini na Afrika kwa ujumla. Ambapo ina mpango wa
kuanzisha jukwaa litakalo wakutanisha wadau wa sekta ya utalii kujadili masuala
yanayowakabili kwa pamoja. Na hii ni kufuatia mafanikio katika uzinduzi wa
ripoti ya utalii mwaka 2017 kwa kushirikiana na Chama cha Hoteli Tanzania,
Shirikisho la Utalii Tanzania, wamiliki wa hoteli, wataalamu mbalimbali, pamoja
na mchango wa ripoti tofauti za ndani na nje ya nchi.
Uzinduzi wa awamu ya
kwanza ya tunzo hizi zilizofanyika mwaka 2016 ulikuwa ni kuhakikisha kujizatiti
kwa Jumia Travel katika kuboresha huduma za usafiri Afrika, kuzifanya sherehe
hizo kama mojawapo ya matukio muhimu kwenye sekta ya usafiri na utalii kwenye
kila nchi. Kwa mwaka huu, tunzo hizi zilifanyika sambamba kwenye miji 6 Afrika
ikiwemo Dar es Salaam (Tanzania), Algiers (Algeria), Dakar (Senegal), Abidjan
(Ivory Coast), Accra (Ghana), Douala (Cameroon) na Kampala (Uganda). Wakati Kenya
na Nigeria zitafanya sherehe zao mnamo Februari mosi, 2018.
Hoteli zilizokuwa zikiwania
tunzo kwenye vipengele tofauti ni pamoja na: Hotel Slipway, Harbour View Suites, Hong Kong Hotel, Peacock Hotels
(City Centre), Amaan Bungalows, Hotel White Sands: The Beach Resort, Mazsons
Hotel, Jafferji House & Spa, Golden Tulip Zanzibar Boutique Hotel, Venus
Premier Hotel, The Lodge Tellamande, Sea Cliff Court Hotel and Luxury
Apartments, The Green of Oysterbay, Mount Meru Hotel, Maru Maru Hotel, Ras
Michamvi Beach Resort, na New Africa
Hotel.
Kwa upande wa shirika
bora la ndege washiriki walikuwa ni: KLM,
Fly Emirates, Precision Air, Ethiopian Airways, Air Tanzania, Fastjet, Coastal
Aviation, na Auric Air. Na kwa kipengele cha tovuti bora inayoandika habari
za kitalii nchini ilikuwa na washindani kama vile: Habari za Jamii Blogspot, Corporate-Digest.com, Michuzijr Blogspot,
Zanzinews.com, Malunde.com, Kajunason.com, Robert Okanda Blogspot, Habari24
Blogspot, Njombe Yetu Blogspot, na Tangarahatz Blogspot.
Comments
Post a Comment