Baada
ya pilikapilika za msimu wa sikukuu na sherehe za kuuaga mwaka 2017 na
kuukaribisha mwaka 2018, huu ni muda muafaka kwako wa kujiwekea malengo
mapya.
Malengo
hutofautiana kulingana na kitu gani unataka kukifanikisha ndani ya
kipindi cha muda fulani. Kwa mfano, kuacha kula aina ya vyakula fulani
au vinywaji kutokana na kuvitumia kipindi cha sikukuu; kubana matumizi
ili kukusanya kiasi fulani cha pesa; au kufanya mazoezi ya kutosha ili
kurudia ile hali yako ya zamani kabla ya sikukuu, nakadhalika.
Kukurahisishia baadhi ya malengo ambayo unaweza kujiwekea mwanzo huu wa mwaka, Jumia Travel imemekukusanyia malengo yafuatayo machache ambayo yanaweza kukufaa endapo utayazingatia.
Punguza muda wa kuangalia luninga, soma zaidi vitabu.
Kuna faida nyingi za kusoma vitabu kuliko watu wanavyofikiria kama vile
kuongeza maarifa juu ya masuala mbalimbali, kupata ujuzi pamoja na
kuburudisha. Kwa mujibu wa wataalamu kusoma vitabu huimarisha afya ya
akili yako pamoja na kukuongezea namna ya kuwasiliana na kuwaelewa watu.
Hivyo basi, kama ulikuwa unatumia muda mwingi zaidi kutazama luninga
basi jaribu kuutumia pia kwa kusoma vitabu.
Lala mapema.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ukosefu wa usingizi unaweza
kusababisha hatari ya kupata magonjwa kama vile kisukari, ugonjwa wa
moyo, utapiamlo na msongo wa mawazo. Mwaka huu mpya jaribu kujiwekea
utaratibu wa kulala mapema, weka kengele ya kukumbusha na hakikisha
unaizingitia ili angalau ulale masaa 7 au 8.
Jaribu kuwa mbali na simu yako.
Nadhani unaweza kuwa umeona mara kadhaa namna simu ya mkononi
inavyowafanya watu kutokuwa makini au kuutoa muda wao kikamilifu katika
baadhi ya shuguli. Unaweza kukuta kwenye kusanyiko la familia au kikao
na mtu muhimu lakini simu inakuwa chanzo cha kuondoa umakini. Jaribu
kulidhibiti hilo kwa kuizima kila unapokutana na watu muhimu au tukio
kwa kipindi cha muda fulani au hata siku nzima pia kama ikiwezekana.
Weka akiba.
Hakuna jambo ambalo lina changamoto kama kujiwekea akiba ya fedha.
Wengi wetu hatujui namna ya kudhibiti matumizi ya pesa tunazozipata.
Tunajikuta tunaweka hifadhi ya pesa baada ya matumizi kitu ambacho sio
sahihi. Inashauriwa kwamba weka akiba ya fedha kwanza ndipo utumie kiasi
kilichobakia. Na hakikisha unajitahidi kutumia kiasi ambacho
umekwishajiwekea bajeti ili usiitumie akiba uliyojiwekea.
Punguza muda unaoutumia mitandaoni.
Ni vizuri kutumia muda mtandaoni kwani unakupatia fursa ya kupata
taarifa, maarifa pamoja na kujuana na watu tofauti. Lakini kutumia muda
mwingi huko kunaweza kuwa na madhara kwako bila ya kutarajia. Wataalamu
wamegundua kwamba kutumia muda mwingi mitandaoni kunaweza kuathiri afya
ya akili yako, wanadai kwamba kunaweza kupelekea mtu kutojiamini
kutokana na yale yanayoendelea mitandaoni.
Punguza madeni.
Mwaka huu ufanye usiwe na madeni mengi yasiyo na tija ambayo hunyonya
fedha zako na kukufanya kutotimiza malengo yako. Hakikisha kwamba
unamaliza kulipa madeni uliyonayo ili uwe huru kifedha. Haukatazwi
kukopa na ni jambo la busara wakati mwingine kwani hukuwezesha
kufanikisha jambo ambalo hauna uwezo nalo kwa wakati uliopo. Lakini
hakikisha unakopa kwa ajili ya jambo la maendeleo na siyo starehe.
Tumia muda zaidi na familia yako.
Inawezekana mwaka ulioisha haukupata muda wa kutosha wa kutumia pamoja
na familia yako badala yake ulikuwa umetingwa na kazi au marafiki. Wengi
wetu huwa tunagundua ni jambo jema kutumia muda na familia hususani
kwenye kipindi cha sikukuu. Unaweza kulibadili hilo kwa kujiwekea
malengo mapema. Unaweza kupanga labda kila baada ya mwezi mmoja, miezi
mitatu au minne.
Tabasamu, kutana na watu zaidi! Kuwa
na furaha ni chaguo lako. Changamoto kwenye maisha lazima zitakuwepo,
lakini ni chaguo lako aidha kuziruhusu zikuathiri au la. Jumia Travel
inaamini kwamba mwaka huu mpya ufanye uwe wa pekee kwa kubadili mtazamo
juu ya maisha yako, kutana zaidi na watu, badilishana mawazo, huwezi
kufahamu kwani kwa kuzungumza zaidi na watu kunaweza kukufungulia
milango ya fursa kwenye maisha yako!
Heri ya mwaka mpya 2018 na uwe wenye mafanikio tele kwako!
Comments
Post a Comment