Na Jumia Travel Tanzania
Siku ya Oktoba 16 dunia huadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambapo
Shirika la Chakula Duniani (FAO) kila mwaka huadhimisha kwa shughuli na
kauli mbiu mbalimbali. Kwa mwaka huu kauli mbiu ni ‘Badili Hali ya
Uhamiaji ya Baadaye: Wekeza Katika Usalama wa Chakula na Maendeleo ya
Vijijini.’ Kwa mujibu wa FAO, dunia inapitia mabadiliko kadha wa kadha
kila kukicha. Watu wengi wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na
sababu tofauti kama vile kuongezeka kwa migogoro na kutokuwepo usalama
wa kisiasa. Lakini njaa, umasikini, na kuongezeka kwa matukio ya hali ya
hewa yanayochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni sababu zingine za
muhimu zinazochangia katika kupelekea watu kuhama.
Miongoni
mwa changamoto kubwa inayowakumba watu siku za hivi karibuni ni katika
upatikanaji wa chakula, matumizi yake na namna ya kudhibiti ili kutoleta
athari katika mwili. Kwa kuwa siku hiyo ni maadhimisho ya ‘Siku ya Chakula
Duniani,’ Jumia Travel ingependa kukushirikisha aina za vyakula vya kupunguza au kuacha kula kabisa kama unataka kupunguza uzito wa mwili wako.
Chipsi.
Kwa wakazi wengi wa sehemu za mijini kama vile jiji la Dar es Salaam,
chipsi ni mojawapo ya chakula kinachotumiwa na idadi kubwa ya watu. Na
hii ni kutokana na upatikanaji wake kwa urahisi karibu kwenye kila
maeneo wanapoishi. Kwa mujibu wa tafiti, chakula hiki kinaongeza uzito
mwilini kutokana na kuwa na kalori nyingi ndani yake na ni rahisi kuzila
nyingi zaidi kwa mpigo. Tafiti pia zinaendelea kwa kuelezea kuwa chipsi
pengine ndiyo chakula kinachochangia kuongeza uzito kuliko chakula
chochote. Hivyo basi, kwa afya yako unashauriwa kuvichemsha kwa maji na
kula badala ya kukaanga.
Vinywaji vyenye sukari nyingi.
Vinywaji vinavyotengenezwa na kuongezewa sukari ili kuwa vitamu
vinatajwa kuwa ni mojawawapo ya vyakula hatari zaidi kiafya duniani.
Vinahusishwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa uzito na vinaweza kuwa
na madhara zaidi mwilini endapo vitatumiwa kwa kiasi kikubwa. Ingawa
vyakula hivi huwa na kalori nyingi lakini ubongo wako hauvitambui kama
ni vyakula vigumu. Kwa hiyo, kama una nia ya dhati kabisa ya kupungua
uzito ni vema ukaachana na vinywaji vya aina hii.
Chokoleti.
Inafahamika watu wengi hupendela chokoleti kutokana na utamu wake
lakini ni hatari sana kiafya. Hutengenezwa kwa kuongezewa sukari nyingi
zaidi, mafuta na unga uliosafishwa zaidi kiwandani kwa kiasi fulani.
Chokoleti zina kalori nyingi huku virutubisho vikiwa ni vichache.
Kipande cha kawaida cha chokoleti kinakadiriwa kuwa na kalori takribani
200-300, huku vipande vikubwa zaidi vinaweza kuwa nazo nyingi zaidi.
Lakini kwa bahati mbaya unaweza kukutana na chokoleti karibu kila mahala
tena zikiwa zimewekwa kwa kutamanisha zaidi ili kukushawishi kununua.
Inashauriwa kama unataka kula chakula kidogo cha kawaida badala yake
kula kipande cha tunda au karanga angalau.
Juisi za viwandani.
Juisi nyingi za matunda unazoziona madukani zinakuwa na virutubisho
vidogo sana ukilinganisha na tunda halisi. Nyingi huwa zinatengenezwa
viwandani na kuongezewa sukari. Kiukweli, huwa na sukari nyingi na
kalori sawa na soda, tena inawezekana vikazidi. Kwa kuongezea juisi za
viwandani hazina nyuzinyuzi ambazo unaweza kuzipata kwenye matunda
halisi. Hivyo basi unashauriwa ni vema ukala tunda kamili badala ya
juisi kwani faida zake haziwezi katu kulingana kama wengi tunavyoamini.
Mikate, biskuti na keki.
Vyakula hivi huongezewa virutubisho vingi ambavyo havina faida mwilini. Tena wakati mwingine huongezewa mafuta hatarishi ambayo
yanahusishwa kuwa chanzo cha magonjwa tofauti. Kwa kawaida vyakula hivi
havishibishi hivyo utatamani kuvitumia zaidi na hivyo kupelekea kula
sumu zaidi.
Baadhi ya vileo (hususani bia). Kwa
kiasi kikubwa pombe hutuongezea kalori nyingi kuliko wanga na protini
mwilini mwetu. Hata hivyo, suala la kunywa pombe na kuongezeka uzito
bado halijathibitishwa moja kwa moja. Unywaji wa pombe wa kawaida
unaweza kuwa hauna matatizo na wakati mwingine huhusishwa na kupunguza
uzito. Lakini kwa upande mwingine, unywaji wa kupindukia hupelekea
kuongezeka kwa uzito wa mwili. Aina ya kileo unachokunywa pia ni kitu
cha kuzingatiwa. Kwa mfano, unywaji wa bia unaweza kupelekea kuongezeka
uzito, huku unywaji wa divai (wine) unaweza kuwa na faida kwa afya ya
mwili.
Aiskrimu.
Chakula hiki ni kitamu sana lakini ni hatari kwa afya ya mwili wako.
Kwani kina kalori nyingi na huongezewa sukari nyingi kwenye utengenezaji
wake. Matumizi kwa kiasi kidogo hayana madhara lakini ni vigumu sana
kujizuia kutokutumia kiasi kikubwa kwa wakati mmoja. Unaweza kutengeneza
wewe mwenyewe nyumbani ili kuweka virutubisho vingi zaidi lakini pia
kujizuia kutumia nyingi zaidi, tenga kiasi kidogo na kingine kifiche ili
kujizuia zaidi.
Pizza.
Chakula hiki ni maarufu sana maeneo ya mijini kutokana na upatikanaji
wake wa haraka lakini sio vizuri kiafya kabisa. Huwa na kalori nyingi na
kutengenezwa kwa kuongezewa virutubisho hatari kwa afya kama vile unga
na nyama zinazochakatwa viwandani.
Kutokana
na makala haya unaweza kuwa umegundua kwamba vyakula vingi huwa
vinatengenezwa viwandani na kuwekewa kemikali nyingi ili kuongezewa
ladha na kutumika kwa muda mrefu zaidi. Jumia Travel ingepependa
kukushauri kula vyakula vya asili zaidi au kupika mwenyewe kwani kwa
kufanya hivyo utakuwa unajitengenezea fursa ya kuepuka magonjwa mengi
zaidi sasa na siku za usoni.
Comments
Post a Comment