Sifa na uzuri wa jiji la Arusha ndizo zinaoufanya mji huo kuwa ni miongoni mwa sehemu ambazo watu wengi wa ndani na nje ya nchi kutamani kuutembelea zaidi. Kwa miaka mingi Arusha imekuwa maarufu kutokana na kuwa karibu na vivutio vya kitalii vya Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Mbali na shughuli za kitalii pia umaarufu wa Arusha ni pamoja na kufanyika kwa shughuli nyingi za kisiasa kama vile uwepo wa Makao Makuu ya Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Mbali na vivutio hivyo pia watu wengi hupendelea kutembelea Arusha kutokana na hali ya hewa yake nzuri ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi. Jumia Travel inaamini kwamba watu wengi bado hawana ufahamu juu ya shughuli mbalimbali za kufanya pindi watembeleapo. Yafuatayo ni mambo ya kuyafanya na kufurahia zaidi muda wako ukiwa jijini hapo.
Mnara wa Azimio la Arusha. Kama ilivyo miji mingi nchini na duniani kunakuwepo na alama ambazo ukiziona tu unajua pale ni sehemu fulani. Kwa Arusha eneo la Mnara wa Azimio la Arusha ni nembo mojawapo ya utambulisho wa jiji hilo na kivutio cha watalii pia. Kihistoria, mnara huo ulizinduliwa mwaka 1977 na chama tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi katika kuadhimisha miaka kumi ya Azimio la Arusha. Mnara huo unapatikana katikati ya mzunguko wa barabara ya Makongoro.
Mnara wa Saa. Kabla ya hata kwenda Arusha ninaamini kwamba akilini mwako utakuwa umejiwekea sehemu za kutembelea na kupiga picha kwa ajili ya ukumbusho. Katikati ya jiji la Arusha, kuna mzunguko wa barabara ambao katikati kuna mnara wa saa. Mnara huu ulijengwa mnamo miaka 1950, na kwa mujibu wa wakazi wa jiji hilo wanadai kwamba umbali wa kutoka eneo hilo mpaka mji wa Cape Town wa Afrika ya Kusini ni sawasawa na kwenda Cairo wa nchini Misri.
Kituo cha utamaduni cha Arusha. Nje kidogo ya mji, barabara ya Arusha kuelekea Dodoma kuna kituo ambacho kimejumuisha makumbusho, mgahawa, sehemu ya viungo vya mapishi na maduka. Ukiwa sehemu hiyo unaweza kutembea, kudadisi na kununua kazi mbalimbali za sanaa nakadhalika. Eneo hilo ni maarufu kwa miaka kadhaa kutokana na watu wengi maarufu kutembelea pale wakiwemo Rais wa zamani wa taifa la Marekani, Bill Clinton na bintiye Chelsea.
Makumbusho ya boma la zamani. Mnamo miaka ya 1900, Wajerumani ambao ndio walikuwa wakoloni wa wakati huo walijenga ngome kwa ajili ya shughuli zao za kiutawala. Sehemu hiyo kwa sasa ni nyumba za makumbusho ya kihistoria. Ukiwa pale utaweza kujifunza mambo mengi ya utawala wao pamoja na historia ya eneo hilo.
Tembelea maduka ya Tanzanite. Tanzania ndiyo nchi pekee duniani yanapopatikana madini aina ya Tanzanite ambayo mwonekano wake ni rangi ya zambarau, na Arusha ndipo yanapochimbwa. Litakuwa ni jambo la kuvutia kwa kutembelea maduka mbalimbali yanayopatikana jijini hapo ili kujionea mwenyewe kwa macho yake na pengine kununua zawadi kwa uwapendao.
Hifadhi ya nyoka ya Meserani. Kwenye hifadhi hii utaweza kujipatia fursa ya kujionea nyoka pamoja na wanyama wengine. Hifadhi hii unaweza kujionea aina za nyoka takribani 50 kutoka sehemu za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Ndani ya eneo hilo pia kuna Makumbusho ya Kitamaduni ya Wamasai, soko la bidhaa za asili na mgahawa kwa ajili ya viburudisho mbalimbali.
Arusha au ‘Geneva ya Afrika’ kama wakazi wake na watanzania kwa ujumla wanavyopenda kuiita inayo mambo lukuki ambayo hayatotosheleza kuelezwa kwenye makala haya. Jumia Travel imekusadia kwa baadhi tu ya shughuli nyingi ambazo unaweza kuzifanya tu ukiwa pale jijini. Lakini vivutio vya kitalii ni vingi ambavyo watanzania wamebarikiwa kuwa navyo hapa nchini.
Comments
Post a Comment