Na Jumia Travel Tanzania
Miongoni
mwa tasnia zinazokua kwa kasi sasa hivi nchini Tanzania ni uandishi wa
mtandaoni au blogu. Kuenea na ukuaji wa matumizi ya mtandao wa intaneti
kumepelekea watu waliokuwa wanatamani kuingia kwenye tasnia ya uandishi
kufungua blogu zao mitandaoni.
Blogu
zinatoa fursa kubwa kwa watu mbalimbali wanaopenda uandishi kuandika
masuala mbalimbali juu ya mada tofauti na kuwashirikisha wasomaji wao
kwa njia ya mtandao. Jumia Travel ingependa
kukufungua macho kwamba miongoni mwa masuala ambayo mpaka sasa
hayajaangaziwa kwa kiasi kikubwa ni pamoja na vivutio vilivyopo sehemu
tofauti za nchi ya Tanzania. Zifuatazo ni baadhi tu ya faida chache za
kuanza kuandika na kuwashirikisha wasomaji wako juu ya maeneo tofauti
unayoyatembelea.
Ni fursa ya kuwashirikisha wasomaji wako sehemu tofauti ulizotembelea. Sio
watu wote wamebahatika kusafiri na kujionea maeneo tofauti mbali na
pale wanapoishi. Zipo sababu nyingi zikiwemo shughuli zao kutowaruhusu,
kutokuwa na kipato kinachokidhi au kuwa na majukumu mengine. Hivyo basi
kama umepata fursa ya kusafiri sehemu mbalimbali kuna haja ya
kuwasimulia wale ambao hawajawahi kufika. Kwa kufanya hivyo utajikuta
bila ya kujijua unatoa elimu, kutoa mwamko na hamasa ya watu juu ya
sehemu hiyo na hata kutembelea siku za usoni.
Kunaweza kuwa chanzo cha kukuingizia kipato.
Unaweza ukaanza kama masihara kuwa unaandika juu ya sehemu
unazotembelea kwa kuwa unapenda lakini huweza kujua kwamba inawezekana
kuna watu wanafuatilia kazi zako na kuzipenda. Matokeo ya kuwa mwandishi
mzuri wa makala za kuvutia na wasomaji wako wakazipenda kunaweza
kukufungulia milango ya biashara. Kampuni au mashirika mbalimbali
yanaweza kupendezewa na kazi zako na kutaka kuzitumia au wakakulipa ili
uandike kwa ajili yako. Kwa nchi ambazo zimeendelea hususani za Ulaya,
Marekani na Asia wapo waandishi wengi wa namna hii wanasafiri na
kuandika vile wanavyoviona na kujiingizia kipato cha kutosha na
kuendesha maisha yao. Mbali na njia hiyo yapo pia makampuni, mashirika
au wafanyabiashara watakaokutafuta kutaka kutangaza kupitia blogu yako.
Kenya wenzetu wamekwishaanza na wanafanyaa vizuri hivyo ni wakati sasa
kwa watanzania nao kuchangamkia fursa hii.
Blogu yako inaweza kutumika kama sehemu ya kutoa elimu.
Ukiwa ni mwandishi mzuri na uliyobobea kwenye sekta unayoiandikia kuna
fursa kubwa ya kujijengea uaminifu na mamlaka kwa wasomaji wako.
Ukishajijengea uaminifu miongoni mwa wasomaji wengi basi unakuwa na
mamlaka juu ya kile unachokiandikia na hivyo blogu yako ikatumika kama
kielelezo muhimu. Kwa hiyo ili kufanikiwa katika hili hakikisha kwamba
unaijua vema sekta uliyopo ili kutoa taarifa ambazo watu wataziamini na
kuzitumia.
Uandishi wa kwenye blogu ni miongoni mwa taaluma yenye soko kubwa kwa sasa. Katika
ulimwengu huu wa kidigitali hakuna taasisi, shirika, kampuni au
mfanyabiashara ambaye hayupo mtandaoni. Na hii ni kutokana na uwezo wa
njia hiyo kuwafikia watu wengi na tofauti kwa haraka ndani ya muda
ukizingatia hakuna gharama kubwa zinazotumika. Hivyo basi kwa kuonyesha
uwezo wako wa kuandika unaweza kupata fursa ya kutafutwa na makampuni
yenye uhitaji na watu wenye sifa kama zako. Hivyo basi ni vema kuonyesha
bidii na ueledi mkubwa kwenye kile unachokiandika ili kuwavutia watu
makini.
Ni fursa ya kuitangaza nchi yako.
Bila ya kujijua kwamba kupitia maandiko juu ya sehemu mbalimbali
unayoyachapisha kwa wasomaji wako yanaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye
kuvitangaza vivutio vya nchi yako. Mwisho wa siku simulizi za maeneo
unayokwenda huwavutia watu wa ndani na nje ya nchi na kutamani kwenda
kujionea wenyewe kwa macho yao. Lakini isingekuwa hivyo bila ya nguvu ya
ushawishi wa makala zako. Hivyo ni vema kuandika kwa ustadi mkubwa
ambao utamfanya mtu akisoma ajikute naye ni sehemu ya safari
uliyoipitia.
Kuna
matukio mengi sana ya kuvutia na kusisimua ambayo tunajionea sehemu
mbalimbali tunazozitembelea ambayo kwa hakika kuwasimulia marafiki pekee
haistoshi. Jumia Travel inaamini kwamba kuanzisha blogu yako unaweza
kuushirikisha ulimwengu na kusafiri nawe sehemu mbalimbali za Tanzania.
Ni rahisi, haichukui muda na hakuna malipo ili kufungua blogu, tembelea
tovuti kama vile Blogger au Wordpress ambayo inaweza kukuwezesha kufungua blogu yako bure kabisa.
Comments
Post a Comment