Na Jumia Travel Tanzania
Mitandao
ya kijamii ni huduma zinazopatikana kwenye intaneti ambazo
zinakuwezesha kuwasiliana, kutengeneza maudhui na kuwashirikisha watu
wengine waliopo mitandaoni.
Tofauti na watu wanavyoitumia, Jumia Travel
ingependa kukufunua macho kwamba mitandao ya kijamii imeleta fursa
kubwa ya kutangaza biasahara za aina mbalimbali. Unaweza kuitumia
mitandao hiyo kwa kufanikisha malengo kama vile; kukuza jina na biashara
yako, kuwafahamisha wateja juu ya bidhaa na huduma zako, kujua wateja
wanaichukuliaje biashara yako, kuwavutia wateja wapya pamoja na kujenga
mahusiano thabiti na wateja ulionao.
Faida za kutumia mitandao ya kijamii
Kuwafikia watu wengi.
Badala ya kutegemea wateja kuja moja kwa moja ofisini kwako mitandao ya
kijamii huwafikia mamilioni ya watu sehemu mbalimbali ndani ya muda
mfupi.
Kuwafikia wateja unaowakusudia.
Uzuri wa mitandao ya kijamii ni kwamba hutofautiana kwa aina ya
watumiaji wake kama vile vijana, watu wazima, wanasiasa, wanataaluma na
matabaka mengine. Hivyo hii hutoa fursa kwa mfanyabiashara kulingana na
huduma au bidhaa aliyonayo kujiwekea mkakati wa namna ya kuwafikia.
Unafuu.
Haikuhitaji kuwa na fedha ndipo ufungue akaunti kwenye mtandao wa
kijamii mara nyingi ni intaneti tu. Lakini kama unataka kuitumia kwa
malengo ya kibiashara wamiliki wake hutoza kiasi kidogo cha fedha
ambacho ni rahisi kukimudu.
Kumfikia mtu binafsi.
Mitandao ya kijamii inakuruhusu kujenga ukaribu au kuwasiliana na
wateja wako kwa ukaribu zaidi. Uwezo wa kuyapokea na kuyajibu maswali
yao au kuyasikiliza na kuyafanyia kazi maoni yao vina ushawishi mkubwa
katika kuwafanya wateja kutumia huduma na bidhaa zako.
Uharaka. Ndani ya muda mfupi unaweza kusambaza taarifa juu ya huduma na bidhaa zako kwa watu wengi kwenda sehemu mbalimbali.
Urahisi. Haikuhitaji
kuwa na ‘madigrii’ ya vyuo vikuu ili kuweza kutumia mitandao ya
kijamii. Ni rahisi kuitumia kwa njia mbalimbali kama vile kompyuta,
tabiti au simu za mikononi ambazo watu wengi wanamiliki.
Mitandao mikuu ya kijamii unayoweza kuitumia
Facebook.
Mtandao huu hutoa fursa nzuri kwa wafanyabiashara kuwasiliana na wateja
wao moja kwa moja, kuweka picha na video, kutangaza ofa walizonazo,
bidhaa na huduma mpya na mambo mengine.
Twitter.
Mara nyingi huduma hii hutumika kutuma na kupokea jumbe fupi kutoka kwa
wateja wapya na waliopo. Siku hizi pia hutumika kama nyenzo muhimu kwa
kuweka viungo ambavyo vitawapeleka wasomaji kwenye tovuti.
Youtube.
Mtandao huu hutumika kwa kuweka video tofauti, zinaweza kuwa juu ya
huduma na bidhaa ulizonazo, namna ya kuzitumia pamoja na taarifa
mbalimbali ili wateja wako wazitazame.
Blogu.
Kama mfanyabishara pia unaweza kufungua mtandao huu utakaokupatia fursa
kubwa ya kuwashirikisha wasomaji wako juu ya huduma na bidha zako
pamoja taarifa mbalimbali.
Instagram. Mbali
na mtandao huu ipo mingine pia inayowawezesha watumiaji kuweka na
kuwashirikisha watu wengine picha mbalimbali. Kwa mfano hivi karibuni
Instagram wameuboresha mtandao wao kwa kuwawezesha watumiaji wake kuweka
picha zaidi ya moja. Hivyo kutoa fursa nzuri kwa wafanyabishara kuweka
picha mbalimbali za bidhaa na huduma zao.
Mbali na kuwepo kwa faida lukuki za mitandao ya kijamii, Jumia Travel
ingependa kukuasa kwamba bado unahitajika umakini mkubwa katika nanma
ya kuitumia. Miongoni mwa changamoto unazoweza kukumbana nazo ni pamoja
na kupoteza muda na fedha zako kwa kuwekeza kwenye kitu ambacho
hakitoleta faida, kusambaa kwa habari zisizo sahihi kuhusu biashara yako
kwa wateja na kukumbana na matatizo ya kisheria endapo usipofuata au
kuvunja taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Comments
Post a Comment