Jumia ni chachu kwa ukuaji wa biashara za mtandaoni barani Afrika



Na Jumia Travel Tanzania

Mwaka 2017 kampuni ya Jumia ambayo inajishughulisha na huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao barani Afrika inatimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2012.

Kampuni hiyo ambapo awali ilikuwa ikijulikana kama Africa Internet Group (AIG) pindi inaanzishwa imejikita zaidi na shughuli zake mtandaoni katika maeneo kama ya huduma za chakula (Jumia Food), manunuzi ya bidhaa mbalimbali (Jumia Market), hoteli na usafiri wa ndege (Jumia Travel), makazi (Jumia House), magari (Jumia Cars), matangazo (Jumia Deals) na kazi (Jumia Jobs).

Katika kuzikabili changamoto zinazolikabili bara la Afrika kama vile miundombinu hafifu kama vile usafiri wa barabara na anga, umbali wa maeneo na foleni ndefu za barabarani ambazo husababisha watu kupoteza muda mwingi kufika maeneo mbalimbali zote hizi zinatoa fursa kwa kutumika njia ya mtandao wa intaneti ili kuokoa muda na gharama.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kwamba watumiaji wa mtandao wa intaneti wameongezeka na kufikia milioni 19.86 mwaka 2016 kutokea milioni 17.26 mwaka 2015.

Idadi hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi ambao mpaka hivi sasa wapo zaidi ya milioni 40.17 mwaka 2016 kati ya idadi ya watanzania milioni 50 waliopo sasa.

Je, takwimu hizi zina maanisha nini kwa wadau wa sekta ya mawasiliano, wafanyabiashara na wateja?

Kwa wadau wa sekta za mawasiliano kama vile makampuni ya simu na watoaji huduma za intaneti. Hii ni ishara kwamba watanzania ambao wanatumia mtandao wa intaneti inazidi kuongezeka na haitopungua vivyo hivyo kuendelea kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi. Kuendelea kuimarika kwa uwekezaji kwenye sekta ya mawasiliano kutafungua milango mingi sana kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania hususani kwenye eneo la biashara za mtandaoni ambapo ndipo dunia ilipo sasa. Nasema ilipo sasa kwa sababu wenzetu wan chi za Ulaya, Marekani na Asia walikwishahamia huko muda mrefu tu wakiwa na makampuni makubwa kama vile Amazon, eBay na Alibaba.

Kwa wafanyabiashara. Ili kuongeza ufanisi na kuleta tija kwenye biashara, wafanyabiashara hawana budi kugeukia fursa zinazopatikana kwenye mtandao wa inaneti. Badala ya kutegemea wateja wanaokuja mmoja mmoja dukani inabidi kuhamishia huduma zao mtandaoni ambapo zinaweza kuonekana na kufikiwa na mamilioni ya watanzania kila kona ya nchi. Watanzania wengi hivi sasa wanatumia intaneti kwenye mitandao tofauti ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Youtube, Twitter na kwingineko. Lakini mbali na mitandao hiyo, kuna makampuni yanayowasaidia wafanyabiashara kukuza na kujitangaza zaidi mtandaoni. Kwa mfano Jumia, kupitia tovuti zake inawapa fursa wafanyabiashara kujitangaza na kuonekana zaidi kwa njia za kitaalamu zaidi kitu ambacho mfanyabiashara wa kawaida hawezi kukifanya.

Kwa wateja. Kuenea kwa upatikanaji wa mtandao wa intaneti mpaka kufikia asilimia 83 nchini Tanzania kunamaanisha kwamba huduma nyingi zinaweza kufikika huko. Kwa mfano, wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam hutumia muda mwingi mpaka kufika maeneo ya katikati ya jiji au Kariakoo ambako ndiko maduka mengi yalipo. Lakini kupitia intaneti mteja anaweza kuperuzi huduma na bidhaa kadha wa kadha pamoja na bei zake na kuagiza na kuletewa popote alipo.

Jumia inavyofanya kazi mtandaoni.

Jumia Travel. Mtandao huu umezikusanya sehemu mbalimbali za malazi kuanzia hadhi ya chini mpaka ya juu na kuziweka sehemu moja ili kumrahisishia msafiri pindi anapotafuta malazi. Mteja anafaidika kwa kuweza kuperuzi hoteli zaidi ya 1000 tofauti kutoka kila kona ya nchi, kujua bei za vyumba, upatikanaji wake, mahali zilipo na kuweza kufanya huduma papo hapo hivyo kuokoa muda wa kutafuta hoteli moja baada ya nyingine.
  
Jumia Market. Mtandao huu huwakutanisha wafanyabiashara mbalimbali sehemu moja ambapo huweza kuuza na kununua. Ni rahisi kwa mteja na mfanyabiashara kwani bidhaa za aina mbalimbali mpya pamoja na bei zao huwekwa mtandaoni na wateja kuchaguza zile wazitakazo na kupelekewa pale walipo huku malipo hufanyika pale bidhaa zinapowafikia wateja.

Jumia Food. Kutokana shuguli nyingi kuna wakati watu hukosa muda wa kuacha shughuli zao na kwenda kutafuta chakula. Mtandao huu umetatua changamoto hiyo kwa kuikusanya migahawa na sehemu mbalimbali maarufu zinazotoa huduma za chakula jijini Dar es Salaam na kuwaruhusu wateja kuomba huduma ya chakula na kupelekewa pale walipo.

Jumia House. Makazi ni sekta muhimu hususani kwenye jiji kubwa la kibiashara kama vile Dar es Salaam. Sekta hiyo imekuwa ikikua kwa kasi kwani hata idadi ya watu huongezeka kila kukicha hivyo huduma za vyumba, nyumba, ofisi na viwanja pia huwa na uhitaji mkubwa. Mtandao huu huwapatia fursa watoaji na wahitaji wa huduma hizo kufanya biashara mtandaoni kwa urahisi kabisa.

Jumia Cars. Mtandao huu huwapatia wauzaji na wateja wa magari kupata magari ya matoleo mbalimbali kukutana mtandaoni. Wauzaji huweka magari yao mtandaoni pamoja na bei wanazouza na mawasiliano yao ili wateja waweze kuwafikia kwa urahisi. Hivyo suala la mpaka kumkabidhi dalali linakuwa halipo bali ni mtandao wa intaneti tu.

Jumia Deals. Kwenye majiji makubwa kama vile Dar es Salaam huwa kuna biashara mbalimbali zinazofanyika kwenye maisha ya kila siku. Hivyo basi mtandao huu wenyewe hutoa uwanja mpana kwa watu mbalimbali kuweka mtandaoni bidhaa na huduma mbalimbali wanazozitoa.

Jumia Jobs. Katika dunia ya sasa ambapo kila kitu kinapatikana mtandaoni suala la kutembea na bahasha za kaki kwenda ofisi moja mpaka nyingine kutafuta kazi halipo tena. Kwani siku hizi makampuni na mashirika mbalimbali hutangaza nafasi za ajira mtandaoni. Hivyo basi kupitia mtandao huu ambao hushirikiana na makampuni mbalimbali hupokea, huweka na hupendekeza wafanyakazi kwa nafasi zilizowekwa kwenye mtandao wake. Kwa maana nyingine hufanya kazi ya kuwatafutia watu ajira mabo wamekwishajiunga nao kwa kuwasilisha wasifu wao.

Jumia ni mojawapo tu wa mitandao mingi ya biashara kwa njia ya mtandao ambayo imeona mustakabali mkubwa wa ukuaji wa biashara kwenye sekta hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa bado haijaguswa. Ni fursa kwa wadau wa masuala ya mawasiliano kuitazama kwa umakini sekta hii na watanzania kuelimishwa pamoja na wao wenyewekujitambua kwamba intaneti inaweza kutumika kurahisisha maisha yao ya kila siku badala ya kupoteza data kufuatilia masuala yasiyo na msingi.   

Comments