Na Jumia Travel Tanzania
Ripoti ya Utalii ya mwaka 2017 iliyozinduliwa na Jumia Travel nchini Tanzania imebainisha kuwa idadi ya watanzania wanaotumia simu katika kufanya huduma za hoteli kwa njia ya mtandao imeongezeka na kufikia takribani asilimia 60.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita imebainisha kuwa mpaka kufikia mwaka 2016 watumiaji wa intaneti walikuwa ni zaidi ya milioni 19 kutoka milioni 17 ilivyokuwa mwaka 2015.
Ongezeko hilo limechochewa kwa kiasi kikubwa na kukua na kuenea kwa matumizi ya intaneti nchini (takribani asilimia 40 ya watanzania wamefikiwa na intaneti nchini kote) lakini pia maendeleo ya kasi kwenye sekta ya mawasiliano ya simu ambapo mpaka hivi sasa watanzania zaidi ya milioni 40 wanatumia huduma za simu za mkononi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Meneja Mkaazi wa kampuni hiyo inayojishughulisha na hudumza za hoteli na usafiri barani Afrika, Bi. Fatema Dharsee amesema kuwa kukua kwa sekta hiyo ni ishara nzuri kwa maendeleo ya huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.
“Hakuna anayeweza kubisha kwamba dunia yote kwa sasa imehamia mtandaoni kwani ndiko kwenye urahisi na unafuu mkubwa. Inatia hamasa kuona kuwa watanzania nao hawako nyuma katika kuyapokea na kuendana na mabadiliko hayo. Hivi sasa karibu kila mtanzania ana simu ya mkononi tena ya kisasa ambayo ina uwezo wa kutumia intaneti. Lakini cha kuvutia zaidi ni kwamba kwa namna gani watu wanavyoutumia mtandao huu kwa manufaa yao zaidi badala ya kufanya mambo hayana tija kwao,” alisema Bi. Dharsee.
“Jumia Travel katika ripoti yetu tuliyoiwasilisha inaonyesha kwamba watanzania wanautumia vizuri mtandao wa intaneti kupitia simu zao za mkononi kwenye kufanya huduma zetu. Hii inamaanisha kwamba wameweza kugundua faida zinazotokana na wao kufanya hivyo badala ya kwenda moja kwa moja mahotelini kuulizia huduma. Kupitia mtandao wetu mteja anaweza kujionea huduma za mahoteli zaidi ya 1000 ndani ya wakati mfupi na kuchagulia ile inayomfaa sehemu yoyote ya Tanzania. Kwa kuongezea, ripoti yetu imebainisha kuwa miongoni mwa huduma zinazouliziwa sana na wateja pindi wanapoulizia hoteli ya kwenda ni upatikanaji wa mtandao wa intaneti. Hivyo basi hii ni fursa kubwa kwa watoa huduma kuhakikisha kuwa huduma hii inapatikana kwa uhakika na kuboreshwa zaidi,” alimalizia Bi. Dharsee.
Hii ni mara ya pili kwa Jumia Travel kuwasilisha Ripoti ya Utalii nchini Tanzania ambapo mwaka 2016 walifanya hivyo pia. Miongoni mwa mambo yaliwekwa wazi na ripoti hiyo ni kuendelea kwa kufanya vizuri kwa sekta hiyo kwani mapato yake yameongozeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.9 mwaka 2015 na kufikia 2.1 mwaka 2016. Kiasi hiko kimechangia Dola za Kimarekani bilioni 4.6 mwaka 2016 kutokea 4.2 za mwaka 2015 katika pato la taifa.
Kwa upande wa ajira, katika mwaka 2016 sekta hiyo imeajiri watanzania zaidi ya milioni 1.3 (asilimia 11.6). Idadi hiyo inatarajiwa kukua kwa asilimia 4.6 ndani yam waka huu wa 2017 na kufikia zaidi ya milioni 1.4. Hivyo kuifanya mojawapo ya sekta muhimu katika uchangiaji wa uchumi na pato la taifa kwa ujumla.
Mbali na kuwasilisha ripoti hiyo, Jumia iliwashirikisha habari njema watanzania kuwa inasherehekea miaka mitano tangu kuanza kufanya shughuli zake barani Afrika kwa kuwarahisishia waafrika huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Jumia ambayo inaundwa na kampuni tano (Jumia Travel, Jumia Food, Jumia Market, Jumia Deals na Classified pamoja na Jumia Jobs) pia imeujulisha umma kuwa imefanikiwa kuingia kwenye orodha ya makampuni 50 yanayotoa huduma za mtandaoni duniani kwa mara ya pili mfululizo.
Orodha hiyo ilitolewa na Taasisi ya Kiteknolojia ya Massachusetts (MIT) ya nchini Marekani ambayo huyatambua makampuni 50, yaliyopo tayari na yanayochipukia katika kutengeneza fursa kwa kutumia teknolojia mpya kwenye kutoa suluhu na kukidhi mahitaji ya masoko mbalimbali duniani.
Mwaka huu 2017, Jumia imeshika nafasi ya 44 ukilinganisha na ya 47 kwa mwaka 2016, ikiwa imetajwa kama kampuni iliyojikita zaidi kutatua changamoto zinatokana na huduma kwa njia ya mtandao barani Afrika. Changamoto hizo ni pamoja na barabara zisizopitika kwa urahisi, tabia zisizotabirika za wateja, kukosekana ueneaji wa kutosha wa mtandao wa intaneti ambapo kitakwimu ueneaji wake ni asilimia 27 tu barani kote.
Comments
Post a Comment