Sehemu za kitalii jijini Dar es Salaam




 Na Jumia Travel Tanzania

Umaarufu wa Dar es Salaam kwenye shughuli za kibiashara umelifanya jiji hili kuwa vigumu kwa watu kuvizingatia vivutio vyake vya kitalii. Watu wengi huvifahamu kwa kuviona tu lakini bila ya kujua kihistoria sehemu hizo zina maana sana na wageni huja wakitokea nchi mbalimbali kujifunza.

Ukiachana na ufukwe wa Coco Beach unaopatikana pembezeni mwa bahari ya hindi eneo la Oyster Bay, Jumia Travel ingependa kukufahamisha kwamba unaweza kujifunza na kufurahia mambo mengi pindi utakapotembelea maeneo yafuatayo.

Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni. Makumbusho haya awali yalifunguliwa mwaka 1940 kama kumbukumbu ya Mfalme George wa tano ambapo kihistoria huwarudisha watanzania nyuma walipotokea. Makumbusho haya huonyesha mabaki muhimu ya binadamu wa kale yaliyogunduliwa na Dkt. Leakey aliyoyachimbua kwenye bonde la Olduvai. Wageni wanaweza kujifunza urithi wa kitamaduni kutoka kwa makabila mbalimbali Tanzania pamoja na athari za biashara ya utumwa kipindi cha utawala wa kikoloni. Baadhi ya vitu vingine vinavyopatikana katika makumbusho haya yaliyopo mtaa wa Shaaban Roberts ni zana za jadi, desturi, mapambo na vyombo vya muziki. 


Kijiji cha Makumbusho. Takribani maili 6 kutokea katikati ya jiji, kuna kiji cha makumbusho ambacho kimehifadhi tamaduni za makabila zaidi ya 120 yanayopatikana Tanzania. Wageni wanaweza kuzunguka kwenye vibanda kadhaa vya nyasi vinavyopatikana pale kwenye ukbwa wa takribani hekari 15 na kujionea ufundi wa kijadi katika kuchora, ufumaji na uchongaji. Kijiji hiki kinachopatikana eneo la Kijitonyama, barabara ya Bagamoyo pia huwa na ngoma na michezo ya jadi pamoja shughuli nyingize za kitamaduni.


Sanamu la Askari. Likiwa limetengenezwa kwa shaba sanamu hili ya Askari huonyesha askari akiwa amevalia vazi rasmi lililotumika kipindi cha vita ya Kwanza ya Dunia huku ncha ya mbele ya bunduki (kama kisu) ikiwa imeelekezwa karibu na bandari iliyopo jirani. Sanamu hili huonyesha kama kumbukumbu ya majeshi ya waafrika walioshiriki kupigana kwenye vita ya Kwanza ya Dunia na linapatikana mtaa wa Azikiwe na Samora.

Boma la Kale. Likiwa limejengwa mnamo mwaka 1866 mpaka 1867 na Majid Bin Said, Sultani wa Zanzibar, Boma hili la kale ni jengo lenye umri zaidi ambalo linapatikana kwa sasa jijini Dar es Salaam. Jengo hili lilitumika kuwakarabisha wageni wa Sultani ambaye alikuwa na kasri lake pembeni yake. Vitu vya kuvutia kwenye jengo hili lililopo mtaa wa barabara ya Sokoine ni namna lilivyojengwa kwa ndani vikiwemo mlango wa mbao kutokea Zanzibar na kuta zilizojengwa kutokana na matumbawe.

Kanisa la Mtakatifu Joseph. Jengo hili la Kanisa la Kiroma lilijengwa na wamisionari wa Kijerumani mnamo mwaka 1897 mpaka 1902, kwa kiasi kikubwa ni kivutio kinachoweza kuonekana eneo la karibu na bandarini. Jengo hili kwa ndani limejengwa kwa ufundi na ubunifu wa hali ya juu na kutumia stadi halisi kabiza za kijerumani. Jengo hili ndio Makao Makuu ya kanisa hilo na liinapatikana katika barabara ya Sokoine.  


Kanisa la KKKT Azania Front. Wajerumani walilijenga kanisa la KKKT Azania Front mnamo mwaka 1898. Namna jengo hili lilivyojengwa hususani paa lake kunalifanya kuwa ni nembo ya kivutio jijini Dar es Salaam. Kuna kipindi kanisa hili ndilo lilikuwa kituo kikuu cha shughuli za kimisionari mnamo karne ya 19, kwa sasa ndio makao makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.


Ikulu. Ikiwa imejengwa kwenye miaka ya 1890, jengo la Ikulu ndilo lilikuwa ni makazi ya mwanzo kabisa ya Gavana wa Ujerumani. Mnamo mwaka 1922, Waingereza walifanya maboresho ya jengo hilo maeneo mbalimbali kufuatia kuliharibu katika kipindi cha vita ya Kwanza ya Dunia. Ingawa raia wa kawaida hawawezi kuingia ndani lakini bado linabaki kuwa kivutio kikubwa mtu akipita karibu nalo. Jengo hili linapatikana mtaa wa Luthuli barabara ya kuelekea Kivukoni.   

Kisiwa cha Mbudya. Kisiwa hiki kinapatikana umbali wa dakika kumi kwa mwendo wa boti kutokea Kunduchi kikiwa ni hifadhi ya majinii jijini Dar es Salaam. Ukiwa kisiwani hapa utasahau kabisa pilikapilika za katikati mwa jiji hili kwa kufurahia fukwe safi, michezo ya kwenye maji na kuogelea. Kisiwani haoa kuna vibanda vya kukodisha karibu na ufukwe huku vyakula vya baharini pamoja vinywaji vikipatikana pia. Sehemu hii ni maarufu sana kwa watu wanaopenda kutalii kwa siku moja wakitokea katikati ya jiji.


Kisiwa cha Bongoyo. Takribani maili 4 Kaskazini mwa jiji la Dar es Salaam eneo la Msasani kinapatikana kisiwa cha Bongoyo. Kwa wale wanaopenda kusafiri kwa siku moja na kurudi hii sehemu pekee na ya kuvutia ambayo unaweza kufurahia mambo mengi. Kisiwa kina fukwe safi, michezo ya kwenye maji, pamoja na kujionea aina kadhaa za samaki wa baharini. Nyuma ya kisiwa hiki kuna mibuyu mikubwa ambayo huleta hewa safi kwenye fukwe za kisiwa hiko huku vyakula vya baharini na vinywaji hupatikana kwa ajili ya wanaotembelea. Bongoyo kwa sasa inawezekana kuwa ni miongoni mwa visiwa vinne vinavyotembelewa zaidi kwenye hifadhi za maji jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam ina mambo mengi ya kujifunza ingawa mengi yamezingwa na shughuli za kibiashara zilizotapakaa kila kona. Jumia Travel inaamini kuwa inawezekana unaishi na vivutio vya kitalii karibu nawe lakini ulikuwa haufahamu. Hivyo basi kabla ya kufikiria kwenda mbali kutalii vivutio vingine anza na vilivyomo jijini hapa kwani vipo karibu nawe na haikugharimu sana kuvitembelea.

Comments