Kampuni ya mawasiliano ya simu ya mkononi Halotel wamekiri makosa yalitokea na wameahidi kufuata sheria za nchi katika utoaji wa Huduma kwa wananchi.
Kampuni hiyo imesema, itahakikisha inashirikiana na serikali katika kuboresha huduma za mawasiliano kwa watanzania wote, vijijini hadi mjini.
Mkurugenzi mtendaji wa Halotel Le Van Dai, amesema hayo leo ofisini kwake wakati akitoa ufafanuzi juu ya kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inaikabili kampuni hiyo na aliyekuwa mkurugenzi wao Do Manh Hong.
Amesema, katika kesi hiyo kulikuwa na mashtaka saba, lakini wao walihusishwa katika vipengele viwili tu ambavyo ni kushindwa kutoa taarifa za usajiri wa kampuni ya Unex ambayo ilisajili laini 1000 walizouza na kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kuiuzia kampuni hiyo laini za simu wakati ikiwa haijasajiliwa na kutokuwa na kibali cha TCRA.Kwa kutumia mwanya huo Unex walisimika mitambo ambayo ilisababisha hasara ya milioni 459 kwa serikali.
Amesema, Halotel pamoja na kwamba walikuwa wakishtakiwa pamoja na raia saba wa Pakistani walilipa faini iliyokuwa ikiwahusu wao na hasara hiyo kwa kuwa hawan uhusiano wowote na hao waliobaki.
"Mitambo iliyotumika kuiba mawasiliano ya simu haikuwa yetu, hatukufahamu kama Wateja wetu Unex, walitumia mitambo hiyo kuiba mawasiliano lakini hatuna uhusiano wowote na washtakiwa wengine ambao tumehusishwa nao na hata mitambo iliyotumika siyo ya kwetu" amesema Leo Van Dai.
Ameongeza kuwa Halotel haihusiki kwa vyovyote vile na mashtaka yanayowakabili raia hao wa Pakistani kama vile kusimika mitambo ya mawasiliano kwani wao wanafanya kazi zao kwa kufuata taratibu na sheria za nchini.
Aidha mkurugenzi huyo ametanabaisha kuwa, Halotel imeazimia kufanikisha jitihada za serikali katika kutoa huduma bora za mawasiliano na kuwa wanatarajia kuunganisha vijiji zaidi ya 1500 katika mwaka huu wa fedha kuongeza ufanisi wa huduma za mawasiliano.
Comments
Post a Comment