MAKALA: ASLAY ALIVYOFAULU KUNOGESHA HADITHI TAMU YA MAPENZI NA KISA CHA KWELI KATIKA MAISHA YAKE


Inakaribia takribani miaka miwili sasa tangu msanii wa muziki wa bongo flava, Aslay Isihaka au 'ASLAY' kama anavyojulikana kwa jina la kisanii afiwe na mama yake mzazi mnamo mwezi Septemba mwaka 2015 kwa kusumbuliwa na maradhi ya presha na kisukari katika hospitali ya Temeke.

Kama binadamu wa kawaida Aslay aliguswa sana na msiba ule ukizingitia ni mama yake mzazi na kupitia mahojiano mbalimbali aliyokuwa akiyafanya na waandishi wa habari alionyesha mapenzi ya dhati kwa mzazi wake huyo na jinsi alivyokuwa na mchango mkubwa katika kufanya kwake vizuri kimuziki na maisha yake kwa ujumla.

Kama msanii pia, limekuwa ni jambo la kawaida kuwasilisha hisia tofauti pamoja na matukio wanayokumbana nayo katika maisha yao ya kila siku, Aslay alitoa wimbo wa pamoja na wasanii wenzake wa kundi la YAMOTO BAND chini ya lebo ya MKUBWA NA WANAWE uliokwenda kwa jina la 'MAMA' ambapo walimshirikisha Zena.


Katika wimbo huo wasanii hao kama linavyojinadi jina la wimbo huo 'MAMA,' hawakutoka nje ya mada hiyo, wimbo umeangazia mambo mbalimbali yanayomkabili mama katika malezi ya mtoto tangu akiwa mdogo mpaka anakua, naye Zena ambaye amechukua nafasi ya mama ameitumia nafasi hiyo vilivyo kuelezea changamoto anazokumbana nazo mzazi.

Lakini katika wimbo huu ambao ameufanya ASLAY siku za hivi karibuni unaokwenda kwa jina la "ANGEKUONA," kuna ufundi na ubunifu wa hali ya juu wa kiusanii ambao ameutumia msanii huyu na anastahili pongezi kusema ukweli.


Nimesema ni ufundi na ubunifu wa hali ya juu alioufanya katika wimbo huu kwa sababu ni wasanii wachache sana ambao wamekwishafanya kitu kama hiki na kufanikiwa, yaani kuzungumzia kisa cha kweli kwenye kazi zao za sanaa na wasikilizaji wakapata ujumbe unaowagusa na kuburudika ndani yake.

Katika wimbo huu ASLAY ukimsikiliza kwa makini utagundua kuwa anamuimbia mpenzi wake kwa tabia na sifa alizonazo, kutambua hali na uwezo alionao kimaisha lakini bado akamvumilia na kumpenda kwa dhati. Ni kitu nadra kukutana nacho kwenye maisha ya sasa ambapo mapenzi yametawaliwa na pesa kwa kiasi kikubwa. 

Msanii huyu ametumia kiitikio chenye kibwagizo cha 'Angekuona' ambalo pia ndio jina la wimbo wenyewe kuunganisha yale anayoyaimba katika beti zake na masikitiko yake kwa mpenzi wake huyo kutopata fursa ya kukutana na mama yake (mkwewe) ambaye amekwishatangulia mbele za haki.

Hakuna jambo linalosikitisha katika maisha ya kawaida ya binadamu kama kuondokewa na mzazi hususani akiwa amepitia tabu za kila aina katika malezi, lakini pale tu unapoanza kufanikiwa Mwenyezi Mungu anaamua kumchukua. Ni kazi ya Mungu hatuwezi kulaumu, lakini wengi wetu huwa tunatamani sana mzazi/mlezi awe ni sehemu kubwa ya kufurahia mafanikio tunayoyapata.

ASLAY humu anazungumzia kubarikiwa kupata mwanamke mzuri wa tabia ambaye anamuelewa kwa kila hali licha ya kutokuwa na kipato kikubwa, lakini haiishii hapo, anaenda mbele zaidi kwa kuzungumzia zawadi ya mtoto, ambaye ni kweli anaye, na anatamani kama mama yake angekuwepo angemuona, rejea mstari katika wimbo wake huu mpya pale anaposema, "Mama ulipoondoka, huku nyuma imekuja zawadi,,,," ni simanzi sana kama ukijaribu kuingia kwenye akili ya msanii huyu jinsi anavyojisikia.

Kwa ujumla msanii huyu naweza kusema kuwa amefanikiwa sana kiusanii kwenye wimbo huu kuonyesha uwezo wake wa kisanii kuhusisha kazi ya utunzi pamoja na matukio ya kweli katika maisha yake na mashabiki wakaburudika.

Kwangu mimi nikiusikiliza wimbo huu napata hisia mbili tofuati kwa wakati mmoja; FURAHA na HUZUNI. Sijui wewe????

FURAHA; ni kupitia beti za wimbo huu ambapo anamuimbia mpenzi wake kwa maneno matamu aliyoyapangilia kwa ustadi mkubwa yakiwa yanasindikizwa na mrindimo mzuri wa midundo na sauti yake ya kuvutia. Sidhani kama kuna mwanamke ambaye hatofarijika kusikia maneno hayo kutoka kwa mwanaume wake na pia ni fahari kwa mwanaume kutambua kuwa kati ya watu zaidi ya bilioni 7 wanaoishi kwenye uso wa dunia hii kuna mtu mmoja anayempenda na kumthamini kwa dhati licha ya kutambua hali aliyokuwa nayo.

HUZUNI; inakuja pale kwenye maneno aliyoyatumia kwenye kiitikio cha wimbo huu ambapo ASLAY anaimba kwa masikitiko makubwa sana kwamba licha ya hayo yote anayoyafurahia katika maisha yake kwa sasa, yaani kumpata mwanamke mzuri na sifa alizokuwa anazitaka pamoja na zawadi ya mtoto, lakini mama yake mzazi hakupata fursa ya kuungana naye kuyafurahia hayo yote.

Ni kazi nzuri aliyoifanya msanii huyu katika muziki wa bongo flava na ninaamini huu unaweza kuwa ndio wimbo bora kwa mwaka huu uliozungumzia kisa cha kweli lakini ukiwaacha mashabiki wakiburudika.  Kama haujausikiliza wala kuutazama basi fanya hivyo kwani hautonielewa kile nilichokizungumzia humu ndani.

Comments