RAIS DKT. MAGUFULI AMTAKA MAKONDA KUCHAPA KAZI


Rais Dkt. John Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuendelea kuchapa kazi na kwamba yeye hafanyi kazi kwa kusikiliza maneno ya watu kwenye mitandao kwasababu yeye ndiyo Rais wa nchi hii.
Ameyasema hayo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu za Ubungo (Ubungo Fly Over) jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa kuna baadhi ya watu wanaingilia majukumu yake wakati yeye ndiyo mwenye maamuzi na kwamba hapangiwi kazi ya kufanya kwa sababu anajiamini.
Aidha, Rais Magufuli  amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo badala ya kupoteza muda mwingi kufuatilia yasiyokuwa ya msingi kwenye mitandao.
“Watu wa Dar es Salaam tumejielekeza sana kwenye masuala yasiyokuwa na msingi ambayo hayasaidii maendeleo, ningefurahi sana huko kwenye mitandao kama tungekuwa tunajadili jinsi ya kufanya mambo ya maendeleo,”amesema Rais Magufuli.
Vile vile Rais Magufuli amesema kuwa, yeye anaandikwa sana kwenye mitandao lakini kamwe hatotetereka bali ataongeza kasi ya kufanya kazi.
Hata hivyo, amesema kuwa kuna baadhi ya watu wanadiriki hata kumpangia kazi za kufanya, wakati yeye ndiye anayejua kazi zote zinazomuhusu.

Comments