Na Jumia Travel Tanzania
Hivi kuna mkazi yeyote wa jiji la Dar es Salaam ambaye ni mgeni wa adha zitokanazo na mvua zinazonyesha? Sidhani kama kuna mtu yeyote hafahamu ya kwamba mvua ikinyesha kutakuwa na foleni zisizokwisha, barabara na mitaa tofauti jijini kujaa maji, mafuriko na matamko kadha wa kadha kutoka kwa viongozi wa serikali kuwataka wananchi wahame mabondeni.
Lakini ni wangapi wametafakari watawezaje kukabiliana na mvua zitakaponyesha? Zipo mbinu nyingi tu ambazo Jumia Travel inakushauri uzizingatie ili kipindi cha mvua nyingi za Dar es Salaam kwako kiwe ni cha kawaida katika mwaka.
Amka mapema kukabiliana na foleni ili uwahi shughuli zako
Hakuna wakati ambao kunakuwa na foleni kubwa na zisizopungua kwa muda mrefu jijini Dar es Salaam kama kipindi cha mvua! Lakini jambo hili sio la kushangaza kwa sababu kila mwaka hali hii inajirudia.
Na hiki ni kipindi ambacho mabosi wengi huchukia sana pengine kuliko vipindi vyote vya mwaka maana visingizio vya wafanyakazi wao kuchekelewa kazini kwa sababu ya mvua huwa haviishi. Kwa hiyo unakabiliana vipi na hali hiyo?
Kwanza kabisa lazima uwe makini katika kuwahi kuamka mapema na pia njia ya usafiri utakayoitumia. Inakubidi kuwahi kuamka mapema sana kama unategemea usafiri wa umma au binafsi. Kwa sababu ukifanya hivyo kama kutakuwa na foleni barabarani basi utaziwahi ukilinganisha na ukichelewa kuingia barabarani. Lakini pia kama unategemea usafiri wa umma, mabasi ya mwendokasi ni mkombozi mkubwa kwenye kipindi hiki. Hivyo kwa maeneo ambayo usafiri huu unapatikana ni vema kuutumia ipasavyo kwa sababu yenyewe hayakai foleni kutokana na kuwa na njia zao pamoja na kupewa kipaumbele.
Nunua vifaa vya kujikinga na mvua
Kutokana na jiji la Dar es Salaam kuwa na vipindi virefu vya jua na joto kali, imekuwa ni nadra sana kuwakuta wakazi wake wana vifaa vya kujikinga na mvua kama vile mwamvuli, koti, sweta au viatu vya mvua. Inashauriwa kuwa na vifaa hivi nyumbani kwako ili kujikinga ifikapo kipindi cha mvua na sio kuanza kufikiria kununua kwani inawezekana usiwe na bajeti hiyo pindi unapovihitaji. Vifaa hivyo ni muhimu kwani hukukinga na baridi, kutolawana, magonjwa na hata kutunza mavazi yako kutokana na maji ambayo huweza kusababisha kuharibika.
Umakini kwenye chombo chako cha usafiri
Kwa wenye vyombo vya usafiri wanajua wenyewe ni kadhia gani wanayokumbana nayo ikifika kipindi cha mvua. Kipindi hiki ni jambo la kawaida kukuta magari kadhaa yamezimika au kukwama barabarani kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi. Lakini pia barabara nyingi huharibika na kutopitika kabisa hivyo kulazimisha chombo chako kupita ni kujitafutia kuingia gharama zisizohitajika siku za usoni. Kama inawezekana tafuta njia mbadala ya usafiri katika kipindi hiki au pita kwenye njia ambazo una uhakika ni salama kwa chombo chako.
Kuwa makini na vifaa vyako vya umeme
Siyo vifaa vyote vya umeme vimetengenezwa vikiwa na uwezo wa kuzuia maji kutokuingia ndani yake. Licha ya makapuni mbalimbali kuja na teknolojia hiyo lakini unashauriwa kuwa makini sana aidha kwa kuvivika vifaa maalumu vya kuzuia maji au kuvikinga kabisa na maji. Kipindi hiki ndicho ambacho wengi hupatwa na majanga ya kuharibikiwa na simu, kompyuta, radio pamoja na luninga huko majumbani.
Kuwa makini na vyakula utakavyokula
Kama huwa unakuwa makini na aina ya vyakula unavyokula basi kipindi hiki inabidi uwe makini zaidi. Mvua zikinyesha jijini Dar es Salaam ndiyo kipindi ambacho pia kunakuwa na mlipuko wa magonjwa kadha wa kadha kama vile kipindupindu. Inashauriwa kula chakula sehemu ambayo unaiamini na inayozingatia usafi wa hali ya juu au kama inashindikana uwe unabeba chakula unachopika mwenyewe au kutokula kabisa.
Tumia muda wako kusoma vitabu
Sio watu wote wana utaratibu wa kusoma vitabu kwenye siku zao za kawaida badala yake wanatazama filamu, kusikiliza muziki, kutoka wikendi au kupendelea kutembea. Lakini katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha, barabara hazipitiki, hali ya hewa ni baridi na sehemu nyingi za starehe au kutembelea zinakosa watu ni vema ukajaribu kusoma vitabu. Amini usiamini kuwa hata kutazama filamu na kusikiliza muziki hufikia mahala vinachosha, hiki kinaweza kikawa ni kipindi kizuri cha kujaribu kitu tofauti, nunua vitabu na usome ili uongeze maarifa.
Hivyo basi tusiifanye mvua ikawa ni kisingizio cha kutofanya shughuli zingine au majukumu mengine yanayotukabili. Kila kipindi huja na changamoto pamoja na fursa zake, ni vema kupambana nazo na kuzitumia ili kusonga mbele.
Comments
Post a Comment