MAMBO 10 YA KUZINGATIA WAKATI WA KUFUNGA

Na Jumia Travel Tanzania

Kwa wakristo wengi nchini Tanzania na duniani kote hivi sasa wapo kwenye kipindi cha mfungo (Kwaresma) ambacho hudumu kwa siku 40. Kipindi hiki ni muhimu sana katika imani yao kwani huwawezesha kuwa karibu na Mungu kwa sala, kujinyima na kufanya matendo mema na ya huruma.


Kuna uwezekano mkubwa kwamba usifahamu mambo ya kuzingatia wakati au pindi unapoifingia kwenye mfungo, Jumia Travel inakusogezea karibu mambo yafuatayo ndani ya kipindi hiki muhimu kwa imani yako.

Panga funga yako
Ni vema ukapanga namna ambayo utafunga ili usiingilie ratiba yako ya shughuli zako za kawaida. Unaweza kuamua kufunga kwa kula kiasi, kutokula aina fulani ya vyakula, kunywa maji pekee au kutokula kwa siku nzima kabisa. Lakini kwa kuwa watu wengi ni waajiriwa, basi zingatia funga yako isiathiri shughuli zako za kila siku.

Hakikisha funga yako haiwakwazi wanaokuzunguka
Katika kipindi hiki cha mfungo hakikisha funga yako umekuwa umeipangilia ili isiingiliane na ratiba za watu wengine. Isije ikatokea kuwa familia yako ikashindwa kufanya jambo lolote, kwa mfano, sherehe, kwa sababu wewe umefunga. Fanya funga yako ndani ya muda uliojiwekea na ikifika muda wa sherehe ujumuike nao.

Waambie watu wachache ambao unaona ni muhimu
Sio lazima kila mtu afahamu ya kwamba umefunga kwani ni siri yako wewe na Mungu. Ingawa inashauriwa kama unaishi na mke au mume ukamfahamisha juu ya hilo. Kumwambia kila mtu kuwa umefunga inaweza kuleta tafsiri tofauti kwa wetu wengine.

Jiepushe na vinywaji vyenye ‘caffeine’
Wataalamu wa afya wanapendekeza kujiepusha na vinywaji vyovyote vile ambavyo ndani yake vina caffeine kwa siku kadhaa kabla ya kuanza kufunga, angalau siku 2 au 3. Baadhi ya watu huumwa na kichwa kwa siku 2 au 3 kutokana na kunywa vinywaji vyenye aina hiyo ya kemikali. Kipindi hiki muhimu sana kuwa makini na afya yako, hususani ya tumbo na kichwa kwani utakuwa unakaa muda mrefu bila ya kula chakula.

Jiepushe na vyombo vya habari
Kama ukikaa mbali na vyombo vya habari kama vile runinga, radio, magazeti pamoja na intaneti kwa muda inaweza kukusaidia kufanya fungo yako iwe na maanda zaidi. Kwa sababu kupitia vyombo hivi unaweza kuona, kusikia au kusoma mambo ambayo yakakuondolea umakini na kupoteza maana ya kufunga kwako.

Jiepushe na mwingiliano na watu mbalimbali
Maingiliano na watu mbalimbali yanaweza kusababisha usiwe makini au yakakutia majaribuni na kuyumbisha msimamo wako. Kuna baadhi ya watu kipindi kama hiki huchuka likizo kazini au kusimamisha shughuli zao kama ikiwezekana ili kutekeleza funga zao.

Jihadhari na hisia zako
Baadhi ya watu hupitiwa na hali ya mabadiliko ya hisia tofauti kipindi cha mfungo. Kuna wakati wanakuwa makini na funga zao lakini wakati mwingine wanayumbishwa. Hivyo basi endapo utaligundua hili mapema basi itakusaidia kwenye funga yako. Muombe Mungu akusaidie upitie vipindi vyote vigumu ndani ya kipindi hiki.

Pata muda mzuri wa kupumzika
Uvivu ni jambo ambalo linapigwa vita na vitabu vyote vya dini, lakini kutingwa na shughuli nyingi siku hizi kumewafanya watu kujisahau kutenga muda kwa ajili ya kumuomba Mungu. Ni vizuri ukatenga muda wako vizuri, ukapumzisha mwili na akili ili kutafakari maana nzima ya funga yako.

Zingatia afya ya mwili wako
Kufunga haimaanishi kuwa usifanye kitu chochote kile kwa ajili ya afya ya mwili wako. Unaweza ukaupa mwili wako mazoezi kwa kutembea kidogo sehemu kadhaa ili kufurahia mazingira tofauti.

Kuwa mtulivu na makini kwa dhamira uliyoikusudia
Kufunga ni kipindi maalumu cha kujifunza neno la Mungu, kutafakari na kusali. Ili kumudu hili, chaguo vifungu vya masomo utakayokuwa unayasoma pamoja na mistari ambayo utakuwa unaikumbuka pindi ukitafakari. Funga siku zote huwa inaambatana na maombi.


Kupitia dodoso hizo Jumia Travel inaamini kwamba funga yako itakuwa ni yenye mafanikio na itakusaidia kwa dhamira yoyote ile uliyojiwekea. Na pengine ikawa ni hatua muhimu ya mabadiliko katika mfumo wako wa maisha kwa kutoyarudia yale ambayo unaona hayakuwa na manufaa kwako.

Comments