Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewataka Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kutoa taarifa kwa haraka zaidi kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili kusaidia kutangaza mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Dkt. Abbas amesema hayo Mkoani Dodoma alipokuwa akizungumza na maafisa habari na TEHAMA katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Amesema kuwa mara baada ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa Habari wana wajibu wa kuweka taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati kwa kuwa malengo ya tovuti hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za Serikali.
“Tukifungua tovuti hizi tunapaswa kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la upashanaji wa habari na taarifa za miradi ya Serikali isisubiri tena michakato, isipokuwa kama kutatokea suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi kutoka katika ngazi za juu katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi
Dkt. Abbas amesema kuwa katika zama za sasa taaluma ya habari inahitaji ubunifu mkubwa katika kuisemea Serikali kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha umma badala ya kutumia njia za kawaida na za kila siku.
“Katika maeneo yetu ya kazi tuna vituo vya redio na televisheni ambazo zinawahitaji Viongozi wetu kufanya nao mahojiano maalum kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali, ni wajibu wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha tunaisemea Serikali” alisema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbas amesema kuwa ubunifu ni siri nyingine ya mafanikio katika suala la upashanaji wa taarifa za Serikali, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuwa mbunifu badala ya kulalamika kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili katika maeneo yao ya kazi ikiwemo ufinyu wa bajeti na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi.
Amesema kuwa Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima utendaji kazi wa kila Afisa Habari katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Mikoa na Wilaya na Mikoa ili kuona ni namna gani ameweza kutoa taarifa za Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.
Aidha, Dkt. Abaas ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya tano imetekeleza na inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya umeme vijijini (REA), na ujenzi wa miundombinu mingine kwa kutumia fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kueleza wananchi utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema kuwa ili taarifa hizo za utekelezaji wa mafanikio hayo ya Serikali ziweze kuwafikia wananchi, ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano kujenga na kuimarisha mtandao wa mawasiliano baina yao pamoja na watendaji wengine katika maeneo yao ya kazi.
Comments
Post a Comment