Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kumpa mfanyabiashara Aliko Dangote, eneo la kuchimba makaa ya mawe na agizo hilo liwe limetekeleza ndani ya siku saba.
Amesema kuwa eneo limegwe kutoka eneo la Ngaka lililopo eneo la Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni hiyo ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Pia ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini, kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo ili kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama.
Aidha, ametoa agizo hilo Mkoani Mtwara kabla ya kuzindua magari 580 ya Dangote yatakayokuwa yakibeba saruji kiwandani hapo na kupeleka sehemu mbalimbali.
“Nia yangu nataka kiwanda hiki kifanye kazi kweli ili ikiwezekana ujenge viwanda vingine, ujenge hata kumi,” amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli amemhakikishia Dangote kuwa, ndani ya siku saba atakuwa amepata kibali cha kuchimba makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji.
Comments
Post a Comment