Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape Nnauye ameshiriki katika hafla fupi ya kutoa kibali kwa kituo cha Redio cha EFM kuruhusiwa kurusha matangazo katika mikoa 10 ya nchini Tanzania.
EFM tangu kuanzishwa kwake imefanya vizuri kwa mkoa wa Dar es Salaama kwa kujizolea wasikilizaji wengi kutokana na ubunifu wa vipindi na kampeni mbalimbali na hivyo kutoa changamoto kwa redio kongwe nchini.
Akiongea mbele ya mgeni rasmi, Mh. Nape Nnauye kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha redio cha EFM na luninga TVE, Meneja Mkuu wa EFM, Bw. Dennis Ssebo amesema TCRA imeipa kipali kituo hicho kuanza kurusha matangazo yake kwenye mikoa tisa ya Tanzania.
“Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imeipa kibali EFM kwenda mikoani na tunaingia kwenye mikoa tisa. Hiyo ndio habari kubwa ambayo Mkurugenzi wa EFM alitaka kuzungumza na wananchi hii leo ni kwamba tumepewa ridhaa ya kwenda kwenye mikoa tisa. Mikoa hiyo ni kama vile; Mbeya, Tanga, Mwanza, Mtwara, Manyara, Singida, Kigoma, Tabora na Kilimanjaro.”
Naye kwa upande wake Waziri Nape amesifia uwekezaji mkubwa uliofanywa na kituo hiko cha redio katika kuhakikisha kinarusha matangazo yenye ubora wa hali ya juu.
“Mnavyoonekana nje sivyo mlivyo ndani. Ndani kuna uwekezaji mkubwa wa teknolojia kubwa na hakika gharama iliyotumika kuwekeza hapa ni kubwa sana, sisi kama serikali tunakupongeza sana na tunakutakia kila la kheri. Na ninakuahidi serikali tutakupa ushirikiano na msaada unaouhitaji kuhakikisha uwekezaji huu unasonga mbele,” amesema Nape.
Comments
Post a Comment