BARCELONA YAISHANGAZA DUNIA. AUBAMEYANG AKIPIGA HAT-TRICK KLABU BINGWA BARANI ULAYA

Jana usiku pia kulikuwa na michezo ya hatua  ya 16 bora ya raundi ya pili ya Klabu Bingwa Barani Ulaya ambapo timu za Barcelona na PSG pamoja na Borussia Dortmund na Benfica zikichuana vikali kutafuta nafasi ya kusonga mbele kwenye robo fainali,



Inawezekana jana mashabiki wa soka duniani waliweza kushuhudia tukio la ajabu katika historia ya soka baada ya timu ya Barcelona kutoka Hispania kutinga hatua ya robo fainali kwa kishindo baada ya kuifunga PSG magoli 6-1 na kufanya jumla ya magoli kuwa 6-5 baada ya hapo awali kupokea kichapo cha magoli 4-0.



Halikuwa tukio la kawaida bali ni ari na uwezo wa kusakata soka ndio uliowafanya kusonga mbele dhidi ya PSG ambao wao walionekana kuridhika na magoli yao 4 waliyoyapata nyumbani kwao. Magoli ya Barcelona yalifungwa na Suarez (dakika ya 3), Lionel Messi (penati ya dakika ya 50), Kurzawa (goli la kujifunga mwenyewe dakika ya 40), Neymar (dakika ya 88 na penati dakika ya 90), na goli la ushindi lililowekwa kimyani na Sergio Roberto dakika ya lala salama, 90. Katika mchezo huo Edinson Cavani alifunga goli la pekee la PSG dakika ya 62 na kufanya upepo wa mchezo kubadilika kidogo.




Katika mchezo mwingine uliochezwa nchini Ujerumani, Mwafrika Pierre-Emerick Aubamayeng (dakika za 4, 61 na 88)anayekipiga katika klabu ya Borussia Dortmund alipiga magoli matatu au hat-trick walipocheza dhidi ya Benfica ya Ureno na kuiwezesha timu yake kusonga mbele huku goli lingine likifungwa na Christian Pulisic dakika ya 59. Ushindi huo wa jana uliwafanya kuwa na jumla ya magoli 4-1 baada ya mchezo wa kwanza kufungwa 1-0 walipokwenda Ureno.





Comments