Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania, (TCRA) imekamilisha kanuni za kuhama na namba ya simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine bila ya kubadili (Mobile Number Portability - MNP), hatua ambayo itawaruhusu watumiaji wa simu za mkononi katika nchi za Afrika ya Mashariki kuwa huru kuchagua huduma ya mtandao wa simu wanaoutaka miongoni mwa makampuni nane ya simu zilizopo nchini huku wakibaki kuwa na namba zao zilezile.
"Mamlaka itazindua huduma hii rasmi kabla ya mwisho wa mwezi au mwanzoni mwa mwezi Machi,” alisema Semu Mwakyanjala, Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA.
Mfumo wa kuhama na namba ya simu unawaruhusu wateja kubakia na namba zao pindi wanapohama kutoka kwa mtoa huduma mmoja kwenda mwingine huku wakibaki na namba zao za simu pamoja na taarifa kama zilivyo.
Kwa mujibu wa TCRA, utaratibu wa kubadili kutoka kampuni ya simu kwenda nyingine utaratibiwa na kudhibitwa na chombo kilichopewa leseni.
Kwa kuongezea, Kanuni za Kuhama na Namba ya Simu zinaupa mamlaka huo mtandao mpya kushughulikia mchakato kwa niaba ya anayejiunga ndani ya siku mbili za kazi baada ya kupokea ombi la kuhama.
“Mchakato wa kuhama utakuwa umeundwa kwa mtindo wa dhana ya kukamilisha kila kitu papo hapo, ambapo mteja ataanza kuwasiliana na mtandao mpya au mtoa huduma kisha huo mtandao utatakiwa kushughulikia mchakato mzima kwa niaba ya mteja.”
Katika nchi yenye watumiaji wa simu za mkononi zaidi ya milioni 40, mchakato wa sasa wa kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine unahitaji usajili wa laini mpya ya kadi ya simu yenye namba tofauti na muda mwingine huhitaji simu mpya kabisa.
Teknolojia ya kuhama na namba ya simu inatarajiwa kuongeza ushindani katika sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi Tanzania, kuboresha huduma za mtandao kwa watoa huduma wa simu za mkononi nchini na kuzisukuma kampuni za simu kupunguza gharama zake ili kubakia na wateja wake.
Zipo kampuni nane zinazotoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi nchini ambazo zitajumuishwa kwenye huduma hii mpya. Kampuni hizo ni MIC Tanzania Ltd ambao wanajulikana kama Tigo, Vodacom Tanzania, Bharti Airtel Tanzania, Tanzania Telecommunications Company (TTCL), Zanzibar Telecom Ltd (Zantel), Smile na Benson Informatics Ltd ambao wanajulikana kama Smart na Halotel.
Barani Afrika, Tanzania imechukua hatua hiyo baada ya nchi kama vile Kenya, Morocco, Misri, Ghana, Nigeria na Afrika ya Kusini, ambazo zenyewe tayari zimekwishaingia kwenye huduma ya kuhama na namba ya simu kwenda mtandao mwingine.
Comments
Post a Comment