DIAMOND KUKUTWA NA KOSA LA KUVUNJA SHERIA ZA BARABARANI: KUNAWEZA KUWE NI FURSA KWA SERIKALI NA WASANII

Imeandaliwa na Trend

Inawezekana wakawa wanaonekana sio kioo tena cha jamii kama ilivyokuwa hapo awali kutokana na kashfa walizonazo lakini wasanii wa Bongo Flava wanaoushawishi mkubwa sana kwenye jamii.

Nimeamua kuandika makala hii fupi kufuatia tukio la msanii wa Bongo Flava, Diamond Platnumz kuitwa kituo cha polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga.



Wito huo ulimtaka msanii huyo kujielezea juu ya kipande kifupi cha 'video' kilichosambaa mtandaoni kikimuonyesha akiimba wimbo yeye pamoja na familia yake wakati akiendesha gari huku akiachia usukani na bila ya kufunga mkanda kitendo ambacho ni kinyume na sheria za barabarani. 

Diamond aliitikia wito huo na kukutana na Kamanda Mpinga ambapo alikuja kuweka wazi kwamba alikutwa na kosa na hivyo kuhitajika kulipa faini pamoja na onyo kali.

Kitendo hiko kiliibua mijadala mbalimbali kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa sababu ndiyo njia pekee ambayo huwafikia watu wengi kwa haraka zaidi. Lakini si tu kupitia mitandao hiyo, pia kupitia kurasa za msanii huyo aliweza kuwahabarisha mashabiki zake juu ya tukio hilo na kuwaasa kutojaribu kufanya jambo lile kwani ni uvunjifu wa sheria.

Ndani ya muda mfupi ujumbe pamoja na picha alizopost Diamond uliweza kuwafikia watu zaidi ya 40,000 ambao hao ni wale tu walioweka alama ya kuonyesha kupenda (like) lile jambo ukiachana na ambao wameona (view) lakini hawakufanya hivyo.



Kwangu mimi hii ni fursa ambayo taasisi nyingine za kiserikali ambayo inaweza kuitumia kupitia wasanii hawa pindi wanapokuwa na kampeni zao na wanataka kuwafikia watu kwa urahisi. Kwa sababu endapo ndani ya muda ule mfupi ni idadi ile ya watu walifikwa na ule ujumbe, je itakuwape kama kampeni ikiwa ni ya muda mrefu?

Ninaamini kuwa wasanii wanapenda sana kushirikishwa kwenye kampeni mbalimbali zinazolenga kuijenga jamii yao ambayo ndio mashabiki wao lakini wanakosa hizo fursa au hawajui pa kuanzia.

Isiwe wasanii wanatumika tu kipindi cha kampeni za kisiasa ili kuwavutia wapiga kura na kisha baada ya hapo wanasahaulika mpaka uchaguzi mwingine ukikaribia. Kwani zipo shughuli nyingi ambazo endapo watashirikishwa zinaweza kuleta mabadiliko.

Kupitia tukio hilo na makala hii, ninaamini wadau wataliangalia suala hili kwa jicho jingine na kuwafanya wasanii wetu watumike katika namna ambayo jamii itafaidika zaidi mbali na kutoa burudani ya muziki tu.  

Comments