- Ongezeko hilo lilikuwa ni la 8%
- Nchi za Kaskazini zaongoza ukuaji kwa 13%, huku za Kusini mwa Jangwa la Sahara idadi ikiongezeka kwa 5%
Na Jumia Travel Tanzania
Idadi ya watalii duniani
imekuwa kwa kiwango cha 7% mwaka 2017 na kufikia idadi ya milioni 1,322, kwa
mujibu wa matokeo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Utalii Duniani (UNWTO).
Kulingana na takwimu
zilizoripotiwa kutoka sehemu tofauti duniani, inakadiriwa kwamba idadi ya
watalii waliowasili duniani kote imeongezeka kwa 7% mwaka 2017. Hii ni ishara
nzuri au zaidi ya kiwango kilichokuwepo cha 4% kilichodumu tangu mwaka 2010,
hivyo kuonyesha matokeo mazuri ndani ya miaka saba.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizopo kwa Afrika ambazo Jumia Travel ingependa kukushirikisha, ukuaji katika mwaka 2017 ulikadiriwa
kuwa wa 8%. Ilijiimarisha kama ilivyokuwa kwa mwaka 2016 na kuwa na matokeo
mazuri yaliyofikia idadi ya watalii milioni 62 kutembelea kutoka mataifa
tofauti duniani. Licha ya changamoto mbalimbali hususani za kisiasa, nchi za
Kaskazini mwa Afrika zilirejea kuwa na matokeo mazuri kwenye sekta ya utalii
ambapo idadi ilikuwa kwa 13%, wakati nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara
zenyewe idadi iliongezeka kwa 5%.
Mwaka 2017 ulitawaliwa
na ukuaji endelevu kwenye maeneo mengi na kwa maeneo yaliyokumbwa na changamoto
miaka iliyopita yaliimarika na kurejea hali zao za kawaida. Kwa kiasi kikubwa
matokeo haya yamepelekewa na mabadiliko kwenye uchumi wa dunia na uhitaji
mkubwa kutoka kwenye nchi nyingine na masoko mapya ya kitalii, hususani
kuongezeka kwa matumizi makubwa kwenye nchi kama vile za Brazili na Urusi
ambazo kwa miaka michache iliyopita zilikuwa zimeshuka kidogo.
“Utalii wa kimataifa
unaendelea kukua na thabiti, na kuifanya sekta ya utalii kuwa imara katika
kuendesha shughuli za maendeleo ya uchumi. Ikiwa ni sekta ya tatu katika kuleta
mapato ya kigeni duniani, utalii ni muhimu katika kutengeneza ajira na ustawi
wa jamii duniani kote,” alisema Katibu Mkuu wa UNWTO Bw. Zurab Pololikashvili
kwenye taarifa hiyo. “Bado tukiendelea kukua lazima tufanye kazi kwa
kushirikiana ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu unainufaisha kila jamii kwenye
eneo walilopo, na tunakuwa sambamba kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu.”
Ukuaji unatarajiwa
kuendelea kwa mwaka 2018
Kasi ya ukuaji imara
uliopo hivi sasa inatarajiwa kuendelea mwaka 2018, tena katika kasi endelevu
zaidi baada ya miaka 8 ya upanuzi wa kutosha kufuatia changamoto za kiuchumi na
fedha mwaka 2009. Kulingana na mienendo ya sasa, matarajio ya kiuchumi na
mtazamo kutoka kwa jopo la wataalamu wa UNWTO, UNWTO inatazamia idadi ya
watalii kimataifa kwenye maeneo mbalimbali duniani kukua katika kima cha 4%
mpaka 5% mwaka 2018. Kwa kiasi fulani hii ni juu kwa 3.5% ya ongezeko la
wastani wa kawaida uliotazamiwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 mpaka
2020 na UNWTO katika utabiri wake wa Utalii Kuelekea 2030. Ulaya na
Amerika zote zinatarijiwa kukua kwa 3.5% mpaka 4.5%, Asia na Pasifiki kwa 5%
mpaka 6%, Afrika kwa 5% mpaka 7% na Mashariki ya Kati kwa 4% mpaka 6%.
Utalii Tanzania katika
mwaka 2017
Mwaka 2017 ulikuwa ni
wenye neema na mafanikio kwa upande wa Tanzania kwani ilishuhudia matukio
makubwa kama vile kuja kwa watu mashuhuri kutembelea vivutio vya kitalii kama
vile; Will Smith (mwanamuziki na mcheza filamu), David Beckham (aliyekuwa
mcheza soka wa vilabu vya Manchester United, Real Madrid, AC Milan na PSG),
Mamadou Sakho (aliyekuwa mchezaji wa Liverpool), Morgan Schneiderlin (mchezaji
wa Everton) pamoja na ziara ya kikosi kizima cha timu ya Everton kutokea ligi
kuu ya Uingereza.
Ujio wa watu hao
mashuhuri nchini Tanzania ulisaidia kuipaisha sekta ya utalii kwani katika
matembezi yao waliweza kushirikisha dunia uzuri wa nchi na vivutio tulivyonavyo
duniani. Na kwa kiasi kikubwa ulizaa matunda kwani wengi zaidi waliendelea
kumiminika.
Mbali na watu hao
mashuhuri pia viongozi mbalimbali wa kiserikali kutembelea kwenye vivutio vya
kitalii nchini kulileta hamasa kwa wananchi pia. Mwezi Oktoba, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu alipata fursa ya
kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Bonde la Ngorongoro ambapo aliwahimiza
watanzania kuendeleza juhudi za kuhifadhi na kutunza mazingira ya eneo hilo ili
kuendelea kunufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Lakini katika mwaka huo
pia tulishuhudia mabadiliko kwenye sekta ya utalii ambapo Mh. Dkt. Hamisi
Kigwangala aliteuliwa na Mh. Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Utalii na
Maliasili ambapo kupitia uongozi wake mpya tunaona mabadiliko na jitihada za
dhati katika kuendeleza sekta hii ambayo ina mchango mkubwa katika pato la
ndani la taifa na ajira.
Kwa upande wa
miundombinu, serikali kwa kiasi kikubwa imeendelea kuimarisha sekta ya
mawasiliano kama vile barabara, reli, maji na anga ambapo imefanya uwekezaji
mkubwa. Sehemu nyingi nchini zimekuwa zinafikika kwa urahisi kutokana na
maboresho ya barabara huku uwekezaji mkubwa ukiwekwa katika ujenzi wa reli na
kuzifufua za zamani.
Yapo mengi ya kuvuna
kutoka kwenye sekta ya utalii kama vile ajira na fedha ambazo zinasaidia kukuza
pato la taifa. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Benki ya Taifa (BoT), mapato
ya nje yaliyotokana na sekta ya usafiri, hususani sekta ya utalii, yameongezeka
kwa zaidi ya ilivyokadiriwa na kufikia shilingi bilioni 128.8. Mapato hayo
yamekuwa na kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2,156.9 katika mwaka ulioshia
mwezi Novemba 2017, kutoka Dola za Kimarekani 2,101.2 mnamo mwezi Novemba mwaka
2016, ambapo imechangiwa na kuongezeka kuja kwa watalii.
Comments
Post a Comment