Na
Jumia Travel Tanzania
Januari 12 ya mwaka huu
wa 2018 Wazanzibari pamoja na Watanzania kwa ujumla watakuwa wakiadhimisha
miaka 54 tangu kutokea kwa mapinduzi Visiwani Zanzibar mnamo Januari 12, 1964.
Mapinduzi ambayo yaliyofanywa na wanamapinduzi wa kiafrika na kupelekea kuung’oa
utawala wa kisultani na kiarabu visiwani humo na kuwa na utawala wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na siku hii
kuadhimishwa kila mwaka, bado kuna watu wengi hawafahamu mambo muhimu kuhusu
historia ya Zanzibar na yaliyopelekea mpaka mapinduzi kutokea. Kutokana na
umuhimu wa siku hii kwa vizazi vilivyopita, vya sasa na vijavyo, Jumia
Travel imekukusanyia mambo
muhimu ambayo huna budi kuyafahamu.
Ikiwa na historia ndefu
ya utawala wa Kiarabu tangu mwaka 1698, Zanzibar ilikuwa ni sehemu ya nchi ya
ng’ambo ya Oman mpaka ilipojitwalia uhuru wake mnamo mwaka 1858 na kuwa chini
ya utawala wake wenyewe wa Kisultani.
Wakati wa utawala wa
Sultani Ali Ibn Said mnamo mwaka 1890, Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa
Waingereza mpaka mwaka 1963 ilipowapatia wanzibar uhuru wao, ingawa haikuwahi
kuwa chini ya utawala rasmi wa moja kwa moja wa dola ya Kiingereza.
Wananchi wa Zanzibar kwa
kiasi kikubwa walikuwa ni mchanganyiko kutoka mataifa mbalimbali kama vile Waarabu,
Wahindi, Waajemi, Washirazi na Waafrika, ambapo waarabu na wahindi ndio kwa
kiasi kikubwa walikuwa wamehodhi ardhi na shughuli kuu na njia za biashara.
Kadri muda ulivyozidi kwenda maingiliano baina ya watu wa mataifa hayo yalizidi
kuongezeka kitu kilichopelekea utofauti baina yao kuanza kufifia.
Hata hivyo, walowezi wa
Kiarabu kama wamiliki wa sehemu kubwa ya ardhi ya visiwani humo ndio walikuwa
ni matajiri kuliko waafrika. Suala hilo pamoja na mambo mengine mengi ni
miongoni mwa sababu zilizopelekea waafrika kuona sababu ya kufanya mapinduzi
ili kuwa na utawala wa haki na usawa visiwani humo.
Kwa upande wa kisiasa,
vyama vikuu visiwani Zanzibar vilikuwa vikiendeshwa na kuungwa mkono kulingana na utaifa
(ukabila), kama vile Waarabu walikuwa wakitawala kwa sehemu kubwa ya chama cha
Zanzibar Nationalist Party (ZNP) huku Waafrika ilikuwa ni Afro-Shirazi Party
(ASP).
Baada ya Zanzibar
kutwaliwa na utawala wa Kisultani wa Oman mnamo mwaka 1698, sehemu ya ardhi
yote visiwani humo iligawiwa kwa wanafamilia wa Kifalme wa Oman, ambapo vizazi
vyao viliendelea kuimiliki mpaka mwaka 1964.
Ingawa sio Waarabu wote
walikuwa ni matajiri kama familia ambazo zilikuwa zikimiliki mashamba ya
karafuu na minazi, hasira ambayo waliyokuwa nayo waafrika ambao walikuwa
wakifanya kazi kwenye mashamba hayo ilipelekea kujisikia hali ya kubaguliwa
kwenye ardhi yao wenyewe. Hususani kwa kisiwa kidogo kama cha Zanzibar ambapo
ilikuwa ni rahisi kuona pengo na utofauti mkubwa kati ya familia tajiri za
kiarabu zilizokuwa zinamiliki ardhi na vijakazi wao masikini wa kiafrika.
Harakati za kutaka uhuru
Visiwani Zanzibar zilianza kutokana na vuguvugu za shughuli za kisiasa ambapo
kwa kiasi kikubwa waafrika hawakuwa wanapata uwakilishi sawa na nafasi bungeni.
Kuanzia mwaka 1961 na kuendelea kulianza kufanyika kwa chaguzi za kisiasa za
kidemokrasia ambapo vyama vikuu vya ASP na ZNP vilikuwa vikichuana vikali.
Chama kilichokuwa
kikiungwa mkono na waafrika wengi cha ASP kilikuwa kikiendelea kuungwa mkono na
kukubalika miongoni mwa waafrika wengi. Katika maeneo mengi kulipokuwa kunafanyika
chaguzi kilionekana kuungwa mkono ingawa matokeo ya uchaguzi yalipotoka
yalikuwa yanaonyesha kushinda sehemu chache.
Sababu hiyo ambayo
ilikuwa ikijirudia mara kwa mara kwenye kila chaguzi ndiyo iliyopelekea
waafrika kuona haja ya kufanya mapinduzi. Mnamo Januari 12, 9164 mapinduzi
yalifanyika visiwani Zanzibar na kumfanya kiongozi wa chama cha ASP, Hayati
Sheikh Abeid Amani Karume kuwa Rais mpya na kiongozi wa nchi.
Mapinduzi hayo
yalipelekea ukomo wa utawala wa kiarabu visiwani Zanzibar wa takribani miaka
200, hivyo kuifanya siku hiyo kusherehekewa kwa maadhimisho maalum na kuwa ni
siku ya mapumziko ya kitaifa.
Comments
Post a Comment