Na Jumia Travel Tanzania
Saratani
ya matiti ni miongoni mwa saratani inayomkumba zaidi mwanamke duniani
na ndiyo inayoongoza kwa vifo vinavyotokana na saratani katika nchi
zinazoendelea, ambapo watu takribani milioni 1.7 mwaka 2012
waligundulika kuwa na ugonjwa huo (kwa mujibu wa taarifa zilizopo hivi
sasa). Viwango vya saratani duniani kwa ujumla vinatarajiwa kuongezeka
kutoka milioni 14 mwaka 2012 na kufikia milioni 20 ndani ya miongo
miwili ijayo, na kuifanya saratani kuwa ugonjwa unaotakiwa kuchukuliwa
tahadhari zaidi.
Mwezi
Oktoba wa kila mwaka dunia huwa imeutenga mahususi katika kukuza
uhamasishaji wa kupambana na ugonjwa wa saratani ya matiti duniani.
Kampeni hizo huungwa mkono na serikali, taasisi na mashirika mbalimbali
duniani kwa kuangazia umuhimu wa kuhamasisha juu ya saratani ya matiti,
kutoa elimu na kufanya tafiti. Miongoni mwa shughuli zinazofanywa katika
mwezi huu ni pamoja na kukuza hamasa kwa watu wengi kadri iwezekanavyo
na kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanyia tafiti toauti za ugonjwa huo.
Miongoni
mwa mambo ya msingi unayotakiwa kuyafahamu kuhusu saratani ya matiti ni
pamoja na: saratani ya matiti huwakumba zaidi wanawake; dalili zake ni
pamoja na uvimbe au kuvimba kwa titi, na mabadiliko ya ngozi au chuchu;
sababu zinazoweza kupelekea ni pamoja na kurithi, lakini mitindo ya
maisha, kama vile unywaji wa pombe, unaweza kusababisha kutokea zaidi;
aina mbalimbali za matibabu zinapatikana, zikiwemo upasuaji, tiba ya
mionzi na kimotherapi; uvimbe unaotokea kwenye titi sio saratani, lakini
mwanamke yeyote ili kuchukua tahadhari kuhusu uvimbe au mabadiliko
yoyote inashauriwa kumuona daktari.
Kwa kuwa mwezi huu umelenga kwenye kujenga hamasa juu ya ugonjwa wa saratani ya matiti duniani, Jumia Travel ingependa kukufahamisha juu ya sababu hatarishi zifuatazo zinazoweza kupelekea ugonjwa huo.
Umri.
Hatari ya kuupata ugonjwa huu huongezeka kadri umri nao unavyoongezeka.
Katika umri wa miaka 20, uwezekano wa kupata saratani ya matiti ndani
ya muongo mmoja ujao huwa ni 0.6%. Lakini katika umri wa miaka 70,
takwimu hiyo huongezeka mpaka kufikia 3.84%. Kesi nyingi za ugonjwa wa
saratani zimegundulika baada ya umri wa miaka 50.
Kurithi.
Endapo ndugu wa karibu anaugua au aliwahi kuugua, saratani ya matiti,
hatari ya kuupata ni kubwa zaidi. Wanawake ambao wanabeba jeni aina ya
BRCA1 na BRCA2 wanayo hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti,
saratani ya ovari au zote kwa pamoja. Jeni hizi zinaweza kurithiwa. TP53
ni jeni nyingine ambayo inahusishwa zaidi na hatari ya kusababisha
saratani ya matiti.
Historia ya kuugua saratani ya matiti kipindi cha nyuma.
Wanawake waliowahi kuugua saratani ya matiti kipindi cha nyuma wanao
uwezekano wa kuugua tena, ukilinganisha na wale ambao hawana historia na
ugonjwa huo.
Historia ya saratani ya matiti katika familia. Hatari
kwa mwanamke kupata saratani ya matiti ni kubwa zaidi endapo mama yake,
dada au bintiye (ndugu wa karibu zaidi) au ndugu wengi aidha wa upande
wa mama au baba walikwishawahi kuugua ugonjwa huo. Kuwa na ndugu wa
karibu zaidi wa kiume ambaye aliwahi kuugua saratani ya matiti pia
kunaongeza hatari ya kuupata ugonjwa huo kwa mwanamke.
Uzito wa mwili uliopitiliza.
Wanawake wenye uzito uliopitiliza au utapiamlo hususani baada ya kukoma
kwa hedhi wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti,
pengine kwa sababu ya kiwango kikubwa cha estrojeni (homoni inayohusika
na ukuaji na uwepo wa tabia za kike mwilini). Utumiaji wa kiwango
kikubwa cha sukari pia unaweza kuwa ni sababu.
Matumizi ya pombe.
Matumizi makubwa ya kiwango cha pombe pia huchangia kusababisha ugonjwa
huu. Tafiti zimeonyesha kwamba wanawake wanaokunywa zaidi ya mara 3 kwa
siku wana hatari ya kupata ugonjwa huo mara 1.5.
Matibabu kwa njia ya mionzi kipindi cha nyuma.
Kuwahi kufanya matibabu ya mionzi kwa saratani isiyo saratani ya matiti
kunaongeza hatari ya kupata saratani ya matiti siku za usoni maishani
mwako.
Kutokufanya mazoezi. Wanawake ambao hawafanyi mazoezi ya mara kwa mara pia wanayo hatari ya kupata saratani ya matiti.
Majanga yanayoweza kutokea kazini.
Tafiti zinashauri kwamba sababu zingine kama vile kuvuta sigara,
kufanya kazi mazingira yenye uwepo wa kemikali yanaweza kupelekea
saratani, na pia kufanya kazi kwenye zamu za usiku pia kunaweza
kupelekea saratani ya matiti. Ingawa baadaye watafiti walikuja
kubainisha kwamba kufanya kazi zamu za usiku ni suala ambalo hakuna
uwezekano.
Kwa
kuwa kampeni hii hufanyika duniani kote ikiwemo Tanzania, Jumia Travel
inaamini kwamba kuna hospitali zinafanya kampeni za uhamasishaji juu ya
saratani ya matiti. Ambapo elimu, vipimo na ushauri hutolewa na
wataalamu mbalimbali. Hivyo basi ni fursa kwa kukitumia kipindi hiki
ipasavyo ili kuweza kuujua ugonjwa huu na namna ya kukabiliana nao.
Comments
Post a Comment