Na Jumia Travel Tanzania
Kutokana
na maendeleo ya sayansi na teknolojia binadamu waliyonayo kwa sasa si
jambo la kushangaza kumuwezesha mtu akafanya shughuli zako zote akiwa
yupo sehemu moja ndanin ya muda mfupi.
Kwa
mfano, kwa kutumia simu yako ya mkononi unaweza kutatua changamoto
kadhaa hapo nyumbani kwako kama vile kufanya miamala ya fedha kutoka
benki na kisha kutoa kwa mawakala huduma za fedha, kulipia umeme,
kulipia maji, kulipia king’amuzi, kuagiza chakula, kuagiza usafiri,
kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali.
Lakini
swali ni kwamba, je ni watanzania wangapi wanaiona fursa hiyo
iliyoletwa na teknolojia kama suluhu za changamoto tofauti
zinazowazunguka?
Jibu
ni kwamba ni watu wachache sana walioyapokea maendeleo yaliyoletwa na
teknolojia na kuyatumia katika kurahisisha maisha yao ya kila siku. Ni
jambo la ajabu kuona kwamba mtu ameishiwa na umeme nyumbani kwake lakini
hana suluhu yoyote zaidi ya kwenda kwa mawakala wa huduma za malipo
wakati yeye mwenyewe anao uwezo wa kufanya hivyo kwa kutumia simu yake
ya mkononi.
Zipo
sababu kadha wa kadha zinazopelekea watu wengi kushindwa kuzitumia
huduma hizi ipasavyo mojawapo ikiwa ni elimu ya kuweza kuitumia mifumo
na programu hizo. Ila kwenye suala la elimu sidhani kama ni hoja ya
msingi kwa sababu mifumo takribani yote ni rahisi kwa mtumiaji na
kikubwa zaidi ni kwamba ukiwa unaitumia mara kwa mara inazoeleka kwani
hakuna kinachobadilika.
Kampuni ya Jumia
ambayo imejikita kwenye masuala ya biashara kwa njia ya mtandao barani
Afrika katika nyanja za hoteli na usafiri, manunuzi ya bidhaa, kazi,
makazi, magari, chakula na matangazo mbalimbali imetimiza miaka mitano
(5) tangu kuanzishwa kwake.
Katika
maadhimisho ya sherehe hizo kampuni hiyo imekuwa ikifanya mikutano kwa
njia ya ‘video za moja kwa moja’ na wataalamu na waasisi wa makampuni
mbalimbali ya kiteknolojia duniani. Lengo kubwa likiwa ni kupata
ushauri, uzoefu na mitazamo juu ya ukuaji wa sekta hiyo na mustakabali
wake barani Afrika.
Mojawapo
ya wageni walioalikwa kwenye mfululizo wa ‘video’ hizo alikuwa ni Afisa
Mtendaji Mkuu na mwasisi mwenza wa Andela, Bw. Jeremy Johnson ambayo ni
kampuni iliyoanzishwa kwa madhumuni makubwa ya kuwafunda watengeneza
program barani Afrika (Softwarfe Developers) na kisha kuwaunganisha na
makampuni yenye uhitaji wa wataalamu hao. Mpaka hivi sasa Andela
imefungua matawi yake katika nchi tatu ambazo ni Nigeria (Lagos), Kenya
(Nairobi) na mapema mwaka huu waliongeza tawi lingine jijini Kampala,
Uganda.
Bw.
Johnson katika mazungumzo yake na wafanyakazi wa Jumia alieleza kwamba
mojawapo ya vigezo wanavyoviangalia mpaka wanafikia hatua ya kufungua
tawi nchi husika ni baada ya kufanya utafiti wa kutosha wa maendeleo ya
teknolojia pamoja na shauku ya wananchi wa eneo husika katika kuitumia
ili kutatua changamoto mbalimbali za maisha yao ya kila siku.
Hoja ya msingi iliyoainishwa na mwasisi huyo ambayo Jumia Travel
imeibaini katika mazungumzo yake ni utayari na shauku ya watu kutumia
teknolojia. Kwa hoja hiyo kwa haraka haraka tunaweza kuona kwamba nchi
za Nigeria na majirani zetu wa Kenya wametuacha hatua kadhaa katika
kuyapokea mabadiliko ya kiteknolojia na kuyatumia ipasavyo. Na suala
hilo ni mojawapo ya sababu zinazopelekea makampuni kadhaa kuanzia katika
nchi hizo kabla ya kuvuka mpaka na kuja nchi nyingine ikiwemo Tanzania.
Imefikia
mahali sasa watanzania kubadilika na kuyapokea mabadiliko yanayoletwa
na teknolojia hususani mtandao wa intaneti katika kurahisha maisha yetu
ya kila siku. Zipo huduma nyingi ambazo unaweza ukazipata kwa kubonyeza
tu vitufe vya simu yako mahali popote ulipo na ukazipata. Tukumbuke
kwamba mabadiliko haya yote huja kwa malengo ya kufanya shughuli zetu
ziwe rahisi tofauti na awali na ndiyo maana watu wanaendelea kufanya
uvumbuzi kila kukicha.
Comments
Post a Comment